Hawk-Eye |
Washabiki wa soka wanaofuatilia kwa makini Ligi Kuu ya
Uingereza Premier League,wataanza kuiona teknolojia ya golini ikitumika kwenye
ligi hiyo ifikapo mwezi Januari mwakani baada ya Bodi ya Kimataifa ya Vyama vya
Soka Ulimwenguni (IFAB) kutia tiki matumizi ya teknolojia hiyo katikati ya
wiki.
IFAB(International FA Board)imeingiza teknolojia hiyo kuwa
moja ya sheria zitakazoendesha mchezo huo,na kufungua ukurasa mpya kabisa
katika historia ya mchezo huo unaopendwa zaidi duniani
Mifumo miwili ya teknolojia hiyo ndio iliyopitishwa na
kuruhusiwa kutumika baada ya majaribio mengi ya kisayansi kuwa
yamefanyika.Mifumo hiyo Hawk-Eye na GoalRef inafanya kazi hivi:
HAWK-EYE.
Ni mfumo unaotegemea kamera,ambao ulitengenezwa na kampuni
ya Uingereza ya Hawkeye,na kununuliwa na kampuni ya Kijapan ya Sony mwaka jana,teknolojia
ambayo kwa muda imekuwa ikisaidia maamuzi kwenye michezo ya kriketi na tennis
Kamera 6 au 7 zenye uwezo wa kupiga picha kwa kasi ya ajabu
zitafungwa pande zote mbili za uwanja na nyingine juu,zitakuwa na kazi ya kufuatilia
mpira kila utakapokwenda ndani ya uwanja,kompyuta yenye uwezo wa kusoma taarifa
kwa usahihi wa hali ya juu itakuwa ikipokea picha kutoka kwenye kamera
hizo,kuzitafsiri kwa kasi na hapo hapo kutuma matokeo kwenye kifaa mfano wa saa
ambacho mwamuzi atavaa mkononi kama kinavyoonekana pichani.
Kitu ambacho badomkinatia shaka ni iwapo kamera hizo
zitafanya kazi kwa ufanisi iwapo mpira utakuwa umekumbatiwa na golikipa katika
jitihada za kuwahi kuokoa.
Ingekuwa jambo zuri iwapo picha zinazotoka kwenye kamera
hizo zingerushwa kwenye `replay`(picha za marudio) za kwenye TV pale unapotokea
utata ili na sisi watazamaji tushuhudie jinsi teknojia hiyo inavyofanya
kazi,lakini bahati mbaya FIFA wamesisitiza kuwa picha hizo hazitaoneshwa, si
kwenye TV za uwanjani tu, hata majumbani!Kitu pekee kitakachofanyika ni mwamuzi
wa mchezo kupewa ishara na kifaa alichovaa iwapo mpira utavuka mstari wa goli.
GoalRef |
GOALREF
Teknolojia hii ina mfumo uliobuniwa kwa ushirikiano wa
wataalam wa Denmark na Ujerumani,na imeundwa kwa mfumo wa sumaku maalum ambayo
inauwezo wa kugundua iwapo mpira utavuka mstari wa goli.
Kamba maalum ndogo
ndogo 3 zenye sumaku zinawekwa kwa ndani kwenye mpira eneo kati ya gozi na
blada na mpira utnapo vuka mstari wa goli sumaku hii iliyo ndani ya mpira hutoa
ishara kwenye vifaa maalum (sensor) vilivyowekwa ndani ya nguzo ya juu na zile
mbili za goli.
Zile sensor zinapopata taarifa kutoka kwenye sumaku huwa
kama zimetekenywa na kutoa aina ya mawimbi ya umeme ambayo bila kuchelewa
hudakwa na kompyuta ambayo nayo hupeleka taarifa kwenye kifaa kama saa
atakachovaa mwamuzi mkononi mwake..yote hayo niliyoyataja hufanyika chini ya
sekunde moja!
Hii teknolojia ya GoalRef inatarajiwa kuwa na gharama kidogo
katika kununua na kuifunga kuliko ile ya Hawk-Eye,lakini kampuni
zinazotengeneza mipira bado zinajishauri iwapo ni sahihi kuweka sumaku ndani ya
mipira yao,ila wataalam wa GoalRef
wanaendelea kutoa ushawishi wa kitaalam kuthibitisha kuwa hakuna tatizo.
…………………JE UNA MAONI GANI MSHABIKI WA SOKA?