Pages

 

Sunday, July 14, 2013

BREAKING NEWS:..BASI LA NAJMA LAPATA AJALI DARAJANI RUFIJI

0 comments
Bus la kampuni ya Najma linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Nachingwea, limepata ajali kwenye daraja la Mkapa, Ikwiriri baada ya kugonga pikipiki na kusababisha vifo vya watu wawili papohapo.
Chanzo cha ajali hiyo ni moshi mkali uliotanda kwenye eneo la ajali kutokana na moto uliokuwa unaunguza majani yaliyopo pembezoni mwa barabara ya kusini mara baada ya kumaliza daraja la Mkapa. Basi hilo lilikuwa linatokea Nachingwea kwenda Dar es Salaam.
Watu waliofariki ni wale waliokuwa kwenye pikipiki. Ajali hiyo imetokea majira ya saa 6:40 mchana. Hata hivyo gari hilo halikupinduka isipokuwa imeharibika vibaya sehemu ya mbele. Baada ya ajali hiyo, dereva alisogeza gari kwenye kituo cha polisi cha Ikwiriri na baada ya kutoa maelezo, polisi wameenda eneo la tukio kuchukua maiti.
Mtoa habari hii ni miongoni mwa watu waliokuwa abiria kwenye basi hilo. Namba ya gari ni T 599 CBL aina ya YUTONG
.
Read more...

Saturday, July 13, 2013

BOMOA BOMOA:FAMILIA NZIMA YAJICHOMA MOTO MBELE YA OFISI ZA MANISPAA!

0 comments
Moshi ukiwa umezagaa angani mbele ya jengo la serikali muda mfupi baada ya tukio hilo
Watu watano wa familia moja wamejichoma moto mbele ya ofisi za serikali kwa kile walichodai kupinga mpango wa serikali kubomoa nyumba waliyokuwa wakiishi.

Tukio hilo la kutisha na kusikitisha limetokea magharibi mwa India katika mji wa Rajkot,ulioko katika jimbo la Gujarat na limehusisha mama,watoto wake wawili wa kiume na wake zao.

Hasumati Dalvani mama mwenye umri wa miaka 62,wanawe ,Bharat Masingh,40 na Girish Masingh,38 pamoja na wake zao Asha na Rekha,walijimiminia mafuta ya taa mwilini kabla ya kujilipua.

Familia hiyo imekuwa ikipambana kupinga mpango wa serikali kubomoa nyumba yao waliyoishi kwa miaka 35 sasa,baada ya wakazi wa eneo hilo kulalamika kuwa haikuwa salama.
Mmoja wa majeruhi waliojilipua akisaidiwa kupelekwa hospitali

Watu walioshuhusia tukio hilo walijaribu kuzima moto kwa kutumia vipande vya mapazia,lakini walikuwa wameshachelewa.Watoto  na wake zao walifariki baada ya kufikishwa kwenye Hospitali ya Umma ya Rajkot.

Msemaji wa Hospitali hiyo Dakta Sanjay Shah amesema kuwa majeruhi walifikishwa wakiwa wameungua asilimia 90 hadi 95 ya miili yao,walikuwa katika halimbaya sana.Madaktari walijaribu kuokoa maisha yao lakini ilishindikana.Mama mtu bado yuko hai lakini yuko katika hali mbaya sana

Katika hatua nyingine Meya wa jiji la Rajkot,wakati akitoa rambirambi kwa familia hiyo alisema Manispaa yake haikuwa na mpango wa kubomoa nyumba ya familia hiyo.

Polisi wa huko wamewadaka watu wengine wanne ambao wanadaiwa kuchochea tukio hilo la kujiua.Manispaa tayari imethibitisha kutoa  ya kiasi cha Rupia Milioni 2 na laki 5,sawa na wastani wa Shilingi milioni 66 za kitanzania kama fidia kwa familia hiyo
Read more...

SIRI NJE:MTANZANIA AAMBUKIZWA GONJWA LA ZINAA BBA!!

0 comments
Kwa sauti ya kunong`ona,mshiriki wa kiume kutoka Tanzania katika shindano la Big Brother Africa mwaka huu,Nando,amelalamika kuwa ameambukizwa ugonjwa wa zinaa uitwao Clamydia na mshiriki mwenzie wa kike kutoka Ghana aitwae Selly.

Kwa siku kadhaa sasa,Nando na Selly wamekuwa mbalimbali,jambo ambalo washiriki wenzao pamoja na watu wanaofuatilia shindano hilo wameshindwa kujua kwanini.

Nando alifichua siri hiyo ya kuambukizwa clamydia,gonjwa linaloambukizwa kupitia zinaa,lakini  hakuna mtu mwenye uhakika iwapo Nando anasema ukweli,Hata hivyo angalau kauli ya Nando imeweza kutegua kitendawili cha kwanini washiriki hao hawapatani tena siku hizi,tofauti na ilivyokuwa awali.

Katika siku chache zilizopita Nando amekuwa hajisikii vizuri na muda mwingi amekuwa akiutumia kupumzika kitandani,na hakuna aliyekuwa anajua alikuwa akisumbuliwa na nini.

Iwapo ni kweli Nando ameambukizwa gonjwa hilo,hakuna anaeweza kusema moja kwa moja kuwa Selly ndie aliemwambukiza Nando au Nando alikuwa na gonjwa hilo tangu mwanzo na pia tusipuuze uwezekano wa Nando kuwa anasumbuliwa na tatizo jingine,lakini kwa jinsi mtiriko wa mambo ulivyo,Nando amekuwa hajisiki vizuri na amekuwa akionana na daktari mara kadhaa.Zaidi ya hayo Selly amemdokezea mshiriki mwingine kutoka Botswana, O`neal,kuwa Big Brother amemshauri kutumia kinga anapokuwa mzigoni.Jambo ambalo linaashiria madai ya Nando kuwa na ukweli kiasi fulani

Nando tangu hapo amekuwa akimbughudhi Selly na ilifikia pabaya pale Nando alipokuwa akimdhihaki Selly aliposhindwa kwenye moja ya mashindano ndani ya jumba hilo,hali iliyopelekea Selly kuondoka huku akilia,na kuwaomba washiriki wenzie wam`nominate` ili atoke arudi nyumbani.

Wakati wa mahusiano yao Nando na Selly walikuwa kwenye mahaba mazito na haikuchukua hata siku kabla hawajavunja moja kati ya amri kumi za mwenyezi mungu.Lakini Nando aliwahi kumueleza Selly kuwa yeye hayuko `serious` kwenye mahusiano yao ila anataka kujifurahisha tu.

Read more...

BODABODA TISHIO LA NDOA ZA WATU.

0 comments
Madereva  wa  bodaboda licha ya biashara ya kusafirisha abiria, wamezua tabia nyingine ya kufanya ngono na  wateja wao wa kike, hasa wanafunzi na wake za watu.
Imebainika kuwa baadhi ya madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda wanatumia usafiri huo kuwarubuni na kuwashawishi wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari na kufanya nao ngono.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili jijini Dar es Salaam katika Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondononi, umebaini kuwa wanafunzi wengi wamejiingiza katika vitendo vya ngono baada ya kunaswa na ulaghai wa madreva bodaboda wengi wakiwa vijana wadogo.
Madereva hao wamekuwa wakifanya ngono na wanafunzi, baada ya kuahidi kuwasafirisha bure kwenda na kurudi kutoka shuleni, hasa kwa maeneo ambayo hakuna usafiri wa daladala au eneo lililo mbali na kituo cha basi wakati wa kutoka au kwenda shuleni.
Gazeti hili limebaini kwamba, baadhi ya walimu pia wamejiingiza katika mchezo huo mchafu na kufanya ngono na vijana wadogo wanaoendesha bodaboda.
Madereva hao wanaoonekana katika vituo vya daladala, huwafuata wanafunzi hao wanaosumbuliwa na shida ya usafiri wakikataliwa kupanda daladala makondakta wa daladala hasa wakati wa asubuhi na jioni.
“Njoo asubuhi utaona wanafunzi wanavyohangaika kupata usafiri, mtu amefika kituoni toka saa kumi na mbili hadi saa mbili bado yupo hapa kila basi linalokuja anaambiwa wanafunzi wametosha. Katika mazingira haya kwanini asirubuniwe na mtu wa bodaboda?” alihoji mmoja wa wazazi alijitambulisha kwa jina la Mwambene na kuongeza:
 “Kuna baadhi ya madereva ninawafahamu wana uhusiano na wanafunzi wawili hadi watatu, tena hawachagui mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari, lazima wazazi wawafuatilie watoto wao vinginevyo wanafunzi hawatamaliza masomo.”
Baadhi ya madereva bodaboda walisimulia wanavyowashawishi na kuwanasa wanafunzi, wakikiri kulitumia tatizo la usafiri wa kwenda na kurudi kutoka shuleni kuwapata kirahisi wanafunzi.
Akionekana kuvifurahia vitendo hivyo, mmoja wa madereva wa bodaboda katika kituo cha daladala cha Temeke mwisho, (jina tunalo) alisema baadhi ya wanafunzi wanaona ufahari kupelekwa shuleni kwa pikipiki jambo linalowafanya wawe tayari kukubali kufanya ngono.
“Wapo wanafunzi wanaopenda kuonekana wanatoka katika familia bora, ...hao ndiyo rahisi sana kuwapata, ukimpeleka shuleni mara ya kwanza, mara ya pili basi umemaliza mchezo,” alisema dereva huyo akijinasibu.
Alisema baadhi ya wanafunzi hutoka nyumbani kwao wakiaga wanakwenda shuleni lakini badala yake hukutana na madereva wa bodaboda ambao huwapeleka mafichoni na kufanya nao ngono.

Dereva mwingine wa bodaboda, mkazi wa Keko Machungwa, Elikunda Kileo alikiri kuwepo kwa matukio hayo akisimulia kuwa mmoja wa madereva wa bodaboda alipigwa na wananchi baada ya kukutwa akimtomasa mwanafunzi wa shule ya sekondari akiwa ndani ya mabanda ya kutengenezea samani.
Kwa mujibu wa Kileo, dereva huyo alimhaidi mwanafunzi kuwa angempeleka shuleni, lakini muda mfupi baadaye alimwingiza kwenye banda la mafundi seremala na kuanza kumdhalilisha kwa kumtomasa maeneo mbalimbali ya mwili wake.
“Jamaa aliingia na mwanafunzi kwenye banda la mafundi seremala linalomilikiwa na kaka yake, cha kushangaza tuliona anataka kufanya vitu vya ajabu, maana alianza kumshikashika yule binti, ingawa binti mwenyewe hakuwa na wasiwasi wowote,” alisema Kileo na kuongeza kuwa:
“Mafundi wakamwambia aondoke, lakini jamaa akaanza kuwatukana ndipo walipoamua kumpa kipigo.”
Dereva mwingine wa bodaboda anayefanya kazi Mbezi Msumi alikiri kuwa na uhusiano na wanafunzi wawili na mwalimu mmoja kutokana na kuwapa lifti ya pikipiki mara kwa mara.
“Si unajua tena kaka, mi ninao wawili, mmoja kidato cha pili mwingine cha nne, tena nina mwalimu, wote nawachukua, ingawa wakati mwingine naona aibu kuwa naye kwani yeye ni mkubwa kuliko mimi,” alisema dereva huyo.
Hata hiyo, baadhi ya madereva wa bodaboda waliwatupia lawama wanafunzi kuwa wao ndiyo wanaowashawishi madereva hao kufanya nao ngono.
Renatus Kitwana dereva wa bodaboda anaefanya biashara yake katika kituo cha Ukonga Mombasa, alisema baadhi ya wanafunzi hufika kituoni hapo na kusimama muda mrefu wakiwasubiri ‘watu wao’. “Kuna wanafunzi huja hapa kutafuta pikipiki, lakini wakiwakosa watu wanaowataka watasubiri muda mrefu hadi jamaa watakaporudi kitu kinachoonyesha kuwa nao wanapenda kufanya vitendo hivyo,” alisema Kitwana.
Wanafunzi wananena
Agnes Tarimo, mwanafunzi aliyehitimu kidato cha nne mwaka 2012 katika shule ya sekondari Jangwani, alisema kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wasichana walikuwa wanakwenda shuleni wakiwa na nguo za kubadilisha kwenye mabegi yao kwa ajili ya kutoka shuleni na kuingia mitaani bila kujulikana.
“Kuna wanafunzi wenzetu walikuwa wanabeba nguo za kubadilisha kwenye mabegi yao. Jamaa wa bodaboda wakija wanakwenda nao sehemu wanabadilisha nguo, halafu wanakwenda kufanya mambo yao huko mafichoni,” alisema Agnes.
Naye Mwanaidi Seif mwanafunzi wa kidato cha Tatu, shule ya sekondari Perfect Vision, alisema kuwa  tamaa ya usafiri wa bure (lifti) na chips imewafanya wanafunzi wengi kujihusisha na vitendo vya ngono
 
“Wanafunzi wengi wanatamaa ya kupata vitu vizuri, wengi wamejikuta wakifanya ngono na kupata mimba kwa kupenda kupewa lifti na chipsi,” alisema Mwanaidi.
Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Anthony, Mbagala ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji wa shule, alisema kuwa suala la wanafunzi kuwa na uhusiano na madereva siyo geni na kwamba lipo tangu siku nyingi.
“Ingawa hapa shuleni hatujapata kesi kama hiyo, lakini suala hilo si geni lipo toka siku nyingi na siyo madereva wa bodaboda tu wanaofanya vitendo hivyo hata madereva wa taxi na daladala,” alisema mwalimu huyo. Alisema baadhi ya madereva wanaojihusisha na ‘mchezo’ huo ni watu wazima ambao umri wao ni sawa na wazazi wa wanafunzi wanafanya nao ngono.
“Wengine ni watu wazima kabisa sawa na baba zao... wazazi lazima wawaangalie sana watoto wao hali ni mbaya,” alisema mwalimu huyo.
Wazazi walonga
Meshack Kilave, mkazi wa Tabata ambaye binti yake anasomoma kidato cha kwanza kati shule ya sekondari Magomeni alisema tatizo la wanafunzi kujihusisha kimapenzi na madereva lipo toka siku nyingi na kwamba wanafunzi wanabuni mbinu mpya kila siku za kuwaficha wazazi wao.
“Baadhi ya wanafunzi huaga nyumbani kuwa wanakwenda kwenye masomo ya ziada kumbe wameshatekwa na jamaa wa bodaboda,” alisema Kilave.
Alishauri wazazi kuwafuatilia kwa kuwauliza watoto wanapowabaini kumiliki vitu ambavyo hawakukinunua wazazi.
“Wazazi watawafuatilie watoto wao kwa karibu, watabaini mambo mengi yaliyofichika, badala ya kukaa na kusikia ukiambiwa mwanao ni mjamzito.”
Naye Stumai Ng’ingo, mkazi wa Kongowe alisema ameshtushwa na taarifa za madereva wa bodaboda kufanya ngono na wanafunzi akieleza kuwa ndio kwanza amezisikia taarifa hizo.
“Ndiyo ninasikia kwa mara ya kwanza kuwa madereva wanaweza kufanya hivyo, sijui kama wadogo zangu wanaosoma sekondari wanaweza kupona wasitumbukie mikononi mwa hao jamaa,” alisema Stumai. George Daffa, mkazi wa Mtoni kwa Azizi Ali aliwatupia lawama baadhi ya wazazi kuwa wanachangia watoto wao kufanya vitendo vibaya kutokana na kukosa uangalizi wa kutosha.
“ Baadhi ya wazazi wanahitaji kubadilika, waache tabia ya kudhani wakishawalipia watoto  wao ada basi jukumu la kuwafuatilia limeisha,” alisema Daffa
Read more...

FAMILIA YAPATA KICHAA BAADA YA MGANGA KUWAPA DAWA

0 comments
Mwalimu aliyetumia uchawi kuwaroga wezi, amejikuta akiwaroga shemeji zake waliopata uchizi huko Butiama. Ilikuwa kama simulizi ya kwenye filamu, baada ya mganga wa kienyeji aliyeletwa toka Kenya kuja kuwaroga wezi walioiba nyumbani kwa Mwalimu mstaafu, Raphael Omwando (60), baada ya dawa yake kuwatia uchizi ndugu wa mke mkubwa wa aliyeibiwa.
Mwalimu Omwando ambaye ana wake wawili alivamiwa na wezi waliomwibia pikipiki na mali nyingine, ikiwemo kumjeruhi yeye (Omwando) na mkewe mkubwa. Mke mdogo aliyemuoa hivi karibuni anaishi kwenye nyumba nyingine na hakuweza kuvamiwa na wezi hao, lakini mke mkubwa alipigwa hadi kulazimika kupewa matibabu hospitali.

Watu walio karibu na familia hiyo walisema kutokuelewana kati ya mke mkubwa na mdogo, kulimfanya mke mkubwa aliyejeruhiwa na majambazi kumtuhumu mke mdogo kwamba alishirikiana na majambazi hao.
Filamu hiyo ya familia ilianza kwa ndugu wa mume (Omwando) wanaoishi Kenya, kuleta sangoma kwa ajili ya kubaini wezi waliomwibia ndugu yao.
“Sijui nimefikaje hapa hospitali…maana kumbukumbu zinaishia pale nilipolazimishwa kunywa dawa na mganga wa kienyeji (Sangoma) anayedaiwa kutokea nchini Kenya …ili wezi wa pikipiki na vifaa vya mwalimu mstaafu virudishwe,” hiyo ni kauli ya mmoja kati ya watu wanne waliolazwa hospitali kwa madai ya kurukwa na akili.
Wagonjwa hao ni vijana wanne wa Kijiji cha Kirumi  Kata ya Bukanga, Tarafa ya Makongoro, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara waliolazwa hospitali ya Mkoa wa Mara baada ya kunywa dawa hiyo na kupoteza fahamu huku wakionekana kama mazuzu (Mazombi).

Waathirika
Matiko Joseph (25) anasema yeye alilazimishwa kunywa dawa nyingi pamoja na makapi yake,” …Baada ya kumtajia mganga hivyo akasema ninyi kunyweni nyingi…dawa ilikuwa na ukakasi ilinikereketa sana. Baada ya kunywa niliondoka lakini baadaye hali ikabadilika sana,” anasema na kuongeza,
“Nilishtukia niko hospitali tayari ikiwa ni siku ya pili …Nikisimuliwa ilivyokuwa nazidi kushangaa…huyo mganga alilenga kutuua kabisa….maana wakati anatoa dawa alisema atakayepata madhara hatapona hata akipelekwa wapi mpaka vitu virudi ama fedha…akaondoka kwenda Kenya na hakuacha simu wala jina lake kujulikana,” anasema Joseph huku akipumua kwa harakaharaka.
Tura Joseph (30) anasema wengine walikunywa kidogo lakini wao wana ndugu walilazimishwa kunywa zaidi kwa kile kinachodaiwa kuwa walihisiwa kula njama za kumdhuru shemeji yao, na ndiyo walidhurika zaidi.
Anasema baada ya kunywa alihisi kitu kinamkaba shingoni na kuishiwa nguvu, akawa hoi na kuanza kuongea maneno yaliyowatia shaka, ndugu wakawabeba kwa bajaji hadi hospital

Boniphace Joseph (20)huku akisitasita, anasema ana habari kabla ya kunywa dawa lakini baada ya kunywa hakumbuki kilichoendelea mpaka alipopata fahamu na kuona watu wanamshangaa naye akiwashangaa.
Msira Magesa (17) anasema yeye baada ya kunywa alitoka kwenda kwenye shughuli zake, ghafla akazidiwa na kupewa dawa ya kutuliza maumivu aina ya panadol hali ikazidi kuwa mbaya na kufikishwa hospitali kwa matibabu

Hali ilivyokuwa
Julai 5, majira ya saa 5:15 usiku mwaka huu, Mwalimu mstaafu, Raphael Omwando (60) alivamiwa na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi, wakamkata yeye, mkewe akapigwa na majambazi hao na baada ya kipigo waliiba pikipiki, mabegi ya nguo, sola, sanduku dogo la kuhifadhia nyaraka, simu ya mkononi na vitu vingine.
Omwando kutokana na majeraha aliyoyapata akapelekwa hospitali ya mkoa alikolazwa kwa matibabu, lakini ndugu zake wanaoishi Shirati na wale wanaoishi nchini Kenya baada ya kupata taarifa waliamua kuchukua mganga wa kienyeji kutoka Kenya, ambaye aliwahakikishia kuwa wahusika baada ya saa 3 watarudisha vitu walivyoviiba wakiwa wamejitwisha na pikipiki wakiwa wanaisukuma.
Mganga huyo alieleza dalili za awali zitakazowapata wezi hao kuwa ni kuchanganyikiwa, wengine watakuwa wanakula nyasi kama ng’ombe. Mganga huyo alitoa tangazo kwamba  Julai 9 majira ya saa 9:00 alasiri wanakijiji wote wajitokeze kunywa dawa hiyo ili kuwapata wahusika.

Vituko vyao walikojoleana, kutapikiana
Mmoja wa wauguzi katika hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema, walipofikishwa hapo aliogopa,“ walikuwa wanakojoleana midomoni, wanatapikiana, huku wakiongea lugha za ajabuajabu, tuliogopa maana ni tukio la kwanza kutokea,” anasema.
Anasema walipewa dawa za kuwafanya walale lakini wakaonekana wanaendelea kuongea wengine kukimbia huku wakidai kuna watu wanataka kuwaua, lakini sasa wametulia wanaongea wenyewe.
Shuhuda mwingine Isa Magesa anayemuuguza ndugu yake anasema Matiko, mmoja wa waathirika hao alikuwa akikimbia kasi kwenda nje huku akipiga kelele, “Nililazimika kutoa msaada, nilipomkamata alionekana ana nguvu sana huku akisema…acheni kuniua…hao wanakuja kuniua…nisaidie …wabaya hao, huku akionyesha kwa vidole lakini wao hawawaoni,” anasema.

Mganga Mfawidhi.
Dk Iragi Ngerageza, Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mkoa, anasema vijana hao walifikishwa hapo wakiwa hawajitambui huku ikidaiwa kuwa walipewadawa na mganga wa kienyeji na kuwapokea wakiwa na hali mbaya  na kuwa hali hiyo bado wanaendelea kuichunguza


“Inakuwa vigumu kujua madhara ya hiyo dawa, kama tungeweza kuipata na kupeleka kwa mkemia ingetoa majibu, lakini kwa sasa sisi tunaendeleakuwatibu…lakini ni hatari maana kama walikunywa wakafikia hatua hiyo lazima kuna kitu, ikipatikana itatusaidia,” anasema.

Mke wake akamatwa.
Pilly Esther mke mdogo wa Mwalimu Omwando amekamatwa kwa kuhusishwa na tukio hilo,  kusaidia kumpata mganga aliyehusika na anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Butiama.
Hata hivyo akizungumzia tukio hilo anasema, wakati mume wake anavamia yeye alikuwa kwake na alisikia kelele za mbwa, lakini hakuelewa kilichotokea mwishoni akapigiwa simu na mke mkubwa kuwa wamevamiwa na kuumizwa. “Ndugu wa mume wangu akiwemo mke mkubwa ambaye ni Mjaluo wa kwao walinituhumu mimi kuwa ndugu zangu ndiyo wameiba mali kwa kuwanimeolewa hivi karibuni..au mpenzi wangu wa zamani ndiye amehusika, nilipokataa wakasema wanakuja na mganga kutoka Kenya ambayeanatoa majibu haraka,” anasema.
Anasema mganga aliomba mtendaji kualika wananchi wote lakini akakataa wakafika kama 40 wakiwemo kinamama, lakini kabla ya kutoa dawa akawaanasema wahusika ni kama anawaona hapo anawaomba wasinywe dawa, ajabuwaliopata madhara ni ndugu wa mke mkubwa
Read more...

WALIOZAMBAZA UJUMBE "KIKWETE KAMUUZIA OBAMA" TANZANIA,WAKAMATWA

0 comments

Jeshi la polisi Wilaya ya Geita linawashikilia watu wawili kwa kosa la kusambaza ujumbe kwa njia ya simu za mkononi usemao, "UMEPOKEA SHILINGI 50,000.KUTOKA KWA RAIS KIKWETE KAMA SEHEMU YA MGAO WAKO BAADA YA KIKWETE KUMUUZIA OBAMA NCHI!!"

Kamanda wa polisi mkoani hapo alisema kwamba watu hao walikamatwa baada ya kukutwa msg hizo ktk simu zao za mikononi huku wakiwa wanasambaza kwa watu wengine.
Aliendelea kudai kuwa jeshi la polisi linatoa onyo kwa wale wote wanaowachafua viongozi wa kitaifa kwa njia za ujumbe kwa simu na kwamba watawachukulia hatua kali.
Read more...

VITA UWANJA WA TAIFA JIONI YA LEO

0 comments
LEO, kuanzia saa 9 alasiri,Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inatinga Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kucheza na wenzao, Uganda Cranes, kusaka nafasi ya kucheza Fainali za CHAN, African Nations Championship, zitakachezwa kuanzia Januari 10 hadi Februari 1, 2014 huko Afrika Kusini.

Mashindano haya yalianza kuchezwa huko Nchini Ivory Coast Mwaka 2009 na Tanzania ilishiriki Fainali hizo na yanahusisha Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za ndani ya Nchi zao pekee.
Wachezaji wanaocheza Soka nje ya Nchi zao hawaruhusiwi kushiriki.

KUMBUKUMBU:
CHAN 2009
Tanzania walishiriki Fainali za Kwanza za CHAN Mwaka 2009, wakiwa chini ya Kocha Marcio Maximo, huko Nchini Ivory Coast wakiwa Kundi A pamoja na Wenyeji Ivory Coast, Zambia na Senegal na kumaliza Nafasi ya 3.
Katika Mechi hizo za CHAN Tanzania ilifungwa na Senegal 1-0, kuifunga Ivory Coast 1-0 na kutoka sare 1-1 na Zambia.
AFCON 1980
Tanzania haijawahi kufuzu kucheza Fainali za AFCON tangu Mwaka 1980 walipocheza huko Nchini Nigeria, chini ya Kocha kutoka Poland Slawomir Wolk, wakiwa Kundi moja na Wenyeji Nigeria, Egypt na Ivory Coast ambako walifungwa Mechi ya kwanza 3-1 na Nigeria, 2-1 na Egypt na kutoka 1-1 na Ivory Coast.

Kikosi cha Uganda tayari kipo Nchini kikiwa na Kocha wao Sredojvic Micho na jana kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari Kocha huyo alisema Taifa Stars imekuwa ikifanya vizuri tangu iwe chini ya Kim, na itakuwa na Wachezaji tisa wa Kikosi cha Kwanza kinachocheza Mechi za Mchujo za Kombe la Dunia wakati kwa upande wake atakuwa na Wachezaji wawili tu.
Pia Kambi ya Uganda imekuwa ikilalamikia joto kali la Jiji la Dar es Salaam ambapo wao kwao wamezoea hali ya wastani wa Nyuzijoto 25 wakati wamekumbana na Joto la zaidi ya Nyuzijoto 30.
Kwenye Mechi ya leo Uganda Cranes wanatarajiwa kutumia Mfumo wa 4-3-3 kwa mujibu wa Mdau wao mmoja aliekuwepo wakati Timu hiyo ikifanya Mazoezo wa Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

VIINGILIO:
-Sh. 5,000 kwa Viti vya rangi ya kijani [Viti 19,648]
-Sh. 7,000 Viti vya rangi ya bluu [Viti 17,045]
-Sh. 10,000 Viti vya rangi ya chungwa [Viti 11,897]
-Sh. 15,000 VIP C [Viti 4,060]
-Sh. 20,000 VIP B [Viti 4,160.]
-Sh. 30,000 VIP A [Viti 748]

TAHADHARI:
Washabiki wanakumbushwa kutonunua Tiketi mikononi mwa Watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua Tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
++++++++++++++++++++++++++++++++
Nae Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen, alisema ni muhimu kwao kushinda Mechi hii ili kujiweka katika mazingira mazuri kwa ajili ya Marudiano lakini pia alisema Uganda ndiyo inayoongoza kwa Ubora wa Viwango vya FIFA katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, na hivyo ni changamoto kwao.
Kim Poulsen pia alisema Wachezaji wake tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya Mechi hiyo.
Hapo Jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga, aliitembelea Kambi ya Taifa Stars kwenye Hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam na kuwapa moyo Wachezaji kwa kuwaambia kuwa kiwango walichoonesha kwenye Mechi zilizopita za Mchujo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast kimetoa uhakika wa uwezo wao wa kushindana katika Mashindano yoyote, kwani tayari wameiva.
Rais Tenga, akiwahimiza Wachezaji kupigana kwa ajili ya Tanzania, alitamka: “Kiwango mlichoonyesha katika mechi hizo kila Mtanzania anayewafuatilia amekiona, hivyo hatuna shaka kuwa mtatuwakilisha vizuri kwenye mechi ya kesho dhidi ya Uganda.”

CHAN 2014
RATIBA
KANDA KASKAZINI
(Timu 2 zitafuzu)
05-07/07/13: Tunisia v Morocco
26-27/07/13: Morocco v Tunisia
Algeria v Libya - Imefutwa
Libya watacheza Fainali huko South Africa baada Algeria kujitoa.
KANDA MAGHARIBI A
(Timu 2 zitafuzu)
Raundi ya Awali
30/11/12-2/12/12 : Liberia 0-1 Mauritania; Guinea 0-0 Sierra Leone
14-16/12/12: Mauritania 2-1 Liberia; Sierra Leone 1-1 Guinea
Mauritania wamepita Jumala ya Bao 3-1
Guinea wamepita kwa Magoli ya Ugenini
Raundi ya 1
05-07/07/13: Senegal v Mauritania; Mali v Guinea
26-27/07/13 : Mauritania v Senegal; Guinea v Mali
KANDA MAGHARIBI B
(Timu 3 zitafuzu)
Raundi ya Awali
30/11-2/12/12/12: Burkina Faso 2-1 Togo
14-16/12/12: Togo 0-1 Burkina Faso
Burkina Faso wamepita Jumla ya Bao 3-1
Raundi ya 1
05-07/07/13: Benin v Ghana; Nigeria v Ivory Coast; Burkina Faso v Niger
26-27/07/13: Ghana v Benin; Ivory Coast v Nigeria; Niger v Burkina Faso
KANDA KATI
(Timu 3 zitafuzu)
Raundi ya Awali
Central African Republic v Congo - cancelled
Congo inasonga baada ya kujitoa Central African Republic
Raundi ya 1
05-07/07/13: Cameroon v Gabon; DR Congo v Congo
26-27/07/13: Gabon v Cameroon; Congo v DR Congo
Washindi watatinga Fainali
Mchujo Raundi ya 1
Watakaofungwa Mechi za Raundi ya 1 watapambana kati ya Tarehe 26-28/07/13 na 09-11/08/13 na Washindi wawili kusonga Fainali.
KANDA KATI MASHARIKI
(Timu 3 zitafuzu)
Raundi ya Awali
14-16/12/12: Burundi 1-0 Kenya; Eritrea v Ethiopia ( Ethiopia wamesonga baada Eritrea kujitoa)
06/01/13: Kenya 0-0 Burundi (Burundi wamesonga Jumla ya Bao 1-0)
Raundi ya 1
05-07/07/13: Burundi v Sudan
12-13/07/13: Ethiopia v Rwanda; Tanzania v Uganda
26-27/07/13: Sudan v Burundi, Rwanda v Ethiopia, Uganda v Tanzania
KANDA KUSINI
(Timu 3 zitafuzu pamoja na Wenyeji South Africa)
Raundi ya Awali
30/11-2/12/12 : Mauritius 2-0 Comoros
14-16/12/12: Comoros 0-0 Mauritius
Mauritius yasonga Jumla ya Bao 2-0
Raundi ya 1
23/06/2013: Swaziland 0-1 Angola
29/06/2013: Angola 1-0 Swaziland
Angola yasonga Jumla ya Bao 2-0
26-7/07/13: Mauritius v Zimbabwe; Mozambique v Namibia; Botswana v Zambia
02-04/08/13: Zimbabwe v Mauritius, Namibia v Mozambique; Zambia v Botswana
Raundi ya 2
26-28/07/13 : Mechi za Kwanza
09-11/08/13: Mechi za Pili
Raundi ya 2
Washindi wawili wa Raundi ya 2 wanaungana na Wenyeji South Africa kucheza Fainali.
Mshindi Mauritius/Zimbabwe v Mshindi Mozambique/Namibia
Botswana/Zambia v Angola
Read more...

Friday, July 12, 2013

MAMA KUTOKA KENYA ASABABISHA BINTI MFALME WA SAUDIA KUKAMATWA MAREKANI

0 comments
Picha kutoka kwenye jalada la kesi iliyotolewa na Idara ya Polisi,ikimuonesha Meshael Alayban
Mama mmoja aliyetajwa  kuwa mwana mfalme kutoka Saudi Arabia amekamatwa katika jimbo la Carlifonia nchini Marekani kwa tuhuma za kushiriki biashara ya kuuza watu.
Meshael Alayban, 42, anakabiliwa na mashtaka ya kumlazimisha mama mmoja kutoka Kenya kufanya kazi kwa zaidi ya masaa kumi na sita kila siku, na kumlipa kiasi kidogo cha pesa kuliko walivyokuwa wameafikiana.
Maafisa wa serikali wa wa eneo hilo, wamesema kuwa Bi Alayban alichukua paspoti  ya mama huyo, hatua iliyomfanya atoroke.
Mawakili wa binti mfalme huyo wamesema kuwa kesi hiyo imesababishwa namzozo kuhusu hali ya utendaaji kazi.
Novemba mwaka uliopita, wapiga kura katika jimbo la Carlifonia, waliidhinisha sheria kali dhidi ya watu watakaopatikana na hatia ya kuhusika na ulanguzi wa watu.


Saudi princess charged in Calif. with human trafficking
Binti Mfalme Meshael Alayban (Kulia) akimsikiliza mkalimani wakati alipofikishwa mahakamani jana huko Santa Ana California
Iwapo atapatikana na hatia, Bi Alayban, huenda akahukumiwa kifungo cha miaka kumi na miwili gerezani, adhabau ambayo ni asilimia mia moja zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali, kabla ya wapiga kura kuidhinisha mabadiliko ya sheria hiyo..Waendesha mashtaka wanasema Bi Alayban, ni mmoja wa wake sita wa Mwana Mfalme Abdulrahman bin Nasser bin Abdulaziz al-Saud, mmoja wa watoto wa kiume wa familia ya kifalme nchini Saudi Arabia.

Mama aliezua sakata hilo  Mkenya ambaye jina lake halijatolewa, aliajiriwa na Bi Alayban miaka miwili iliyopita, baada ya kuandikiana makubaliano na shirika moja la kutoa ajira nchini Saudia.
Mama huyo alihaidiwa kulipwa dola elfu moja mia sita kila mwezi na kuwa atafanya kazi masaa manane kila siku kwa siku tano.
Lakini, Bi Alayban amekuwa akimlipa dola mia mbili ishirini kila mwezi na kulazimishwa kufanya kazi kwa zaidi ya masaa kumi na sita kila siku.
Mama huyo kutoka Kenya vile vile amedai, kunyang`anywa paspoti yake ya kusafiria na alirudishiwa muda mfupi tu kabla ya wao kusafiri kwenda Carlifonia na Bi Alayban.
Akiwa Carlifonia, alilazimishwa kufanya kazi nyingi za nyumbani kwa familia nane zilizoishi katika vyumba vinne tofauti, ambako amedai alishikwa kama mateka .
Wakati alipofanikiwa kutoroka, alisimamisha basi moja na kwenda moja kwa moja hadi kituo cha polisi.
Bi Alayban alikamatwa siku ya Jumatano ya juzi na kufikishwa mahakamani jana.
Aliachiliwa huru kwa dhamani ya dola milioni tano na kuamriwa kurejesha pasi ya kusafiria ya mama huyo kutoka Kenya.
Aidha Bi Alayban sasa atavalia chombo maalum ambacho kitatoa maelezo ya mahala aliko na hataruhusiwa kuondoka Marekani hadi kesi hiyo itakapokamilika.
 Waendesha Mashtaka walitaka jaji kumuachilia kwa dhamani ya dola milioni Ishirini au anyimwe dhamana kwa kuwa yeye ni tajiri mkubwa na angeweza kutoroka
Read more...

MALEMA AZINDUA RASMI CHAMA CHAKE

0 comments


Aliyekuwa kiongozi wa vugu vugu la vijana la chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC, Julius Malema amezindua kundi la kisiasa litakalojulikana kama Wapiganiaji wa Uhuru wa Kiuchumi au Economic Freedom Fighters, EFF.
Malema, ambaye alitimuliwa kutoka kwa chama cha ANC, mwaka wa 2012, amesema chama chake cha EFF kinataka zoezi la kugawanya mashamba kuanzisha upya na pia kutaifishwa kwa migodi yote ya madini.
''Tutagawana ardhi sisi zote ukiwa mweusi au mweupe. Lakini ukikataa kugawanya itamaanisha kuwa utalazimishwa kufanya hivyo'' Alisema Bwana Malema.
Ametaja dhamira kuu ya vugu vugu hilo kuwa kupamabana mfumo wa kipebari.
Akiwa amevalia kofia nyekundu iliyo na maandishi ''Amirijeshi Mkuu wa EFF'' Bwana Malema amewaambia waandishi wa habari kuwa chama chake kimebuniwa ili kutetea maslahi ya raia wanaoteseka katika maeneo ya mashinani.

Malema ambaye alikuwa mmoja wa washirika wa karibu wa rais Zuma, kwa sasa ni mmoja wa wakosoaji wakubwa na aliongoza mikakati ya kumuondoa kama kiongozi wa chama cha ANC wakati wa mkutano wa baraza kuu la chama hicho mwaka wa 2012.
Malema ameshutumu rais Zuma kwa kutoimarisha juhudi za kuwasaidia raia weusi wa nchi hiyo ambao ni masikini na waliompigia kura.
Hata hivyo haijabainika ikiwa atawania kiti chochote katika uchaguzi mkuu utakaoandaliwa mwaka ujao, akisema kuwa uamuzi huo utatolewa baada ya mkutano wa baraza kuu la chama hicho cha EFF utakaofanyika mwisho wa mwezi huu.
Wachanganuzi wa kisiasa wanasema idadi kubwa ya raia wa Afrika Kusini, wamepoteza imani na chama cha ANC, ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka wa 1994.
Rais wanasema maafisa wengi wa chama hicho ni wafisadi na hawana nia ya kuimarisha hali ya maisha
Read more...
 
Said Nuhu © 2012 SAID NUHU BLOGS. BLOG IMETENGENEZWA NA BongoClan blog designer nipigie 0658184797