Madereva wa bodaboda licha ya biashara ya kusafirisha
abiria, wamezua tabia nyingine ya kufanya ngono na wateja wao wa kike,
hasa wanafunzi na wake za watu.
Imebainika kuwa baadhi ya madereva wa pikipiki
maarufu kama bodaboda wanatumia usafiri huo kuwarubuni na kuwashawishi
wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari na kufanya nao ngono.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili jijini
Dar es Salaam katika Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondononi, umebaini
kuwa wanafunzi wengi wamejiingiza katika vitendo vya ngono baada ya
kunaswa na ulaghai wa madreva bodaboda wengi wakiwa vijana wadogo.
Madereva hao wamekuwa wakifanya ngono na
wanafunzi, baada ya kuahidi kuwasafirisha bure kwenda na kurudi kutoka
shuleni, hasa kwa maeneo ambayo hakuna usafiri wa daladala au eneo
lililo mbali na kituo cha basi wakati wa kutoka au kwenda shuleni.
Gazeti hili limebaini kwamba, baadhi ya walimu pia
wamejiingiza katika mchezo huo mchafu na kufanya ngono na vijana wadogo
wanaoendesha bodaboda.
Madereva hao wanaoonekana katika vituo vya
daladala, huwafuata wanafunzi hao wanaosumbuliwa na shida ya usafiri
wakikataliwa kupanda daladala makondakta wa daladala hasa wakati wa
asubuhi na jioni.
“Njoo asubuhi utaona wanafunzi wanavyohangaika
kupata usafiri, mtu amefika kituoni toka saa kumi na mbili hadi saa
mbili bado yupo hapa kila basi linalokuja anaambiwa wanafunzi wametosha.
Katika mazingira haya kwanini asirubuniwe na mtu wa bodaboda?” alihoji
mmoja wa wazazi alijitambulisha kwa jina la Mwambene na kuongeza:
“Kuna baadhi ya madereva ninawafahamu wana
uhusiano na wanafunzi wawili hadi watatu, tena hawachagui mwanafunzi wa
shule ya msingi au sekondari, lazima wazazi wawafuatilie watoto wao
vinginevyo wanafunzi hawatamaliza masomo.”
Baadhi ya madereva bodaboda walisimulia
wanavyowashawishi na kuwanasa wanafunzi, wakikiri kulitumia tatizo la
usafiri wa kwenda na kurudi kutoka shuleni kuwapata kirahisi wanafunzi.
Akionekana kuvifurahia vitendo hivyo, mmoja wa
madereva wa bodaboda katika kituo cha daladala cha Temeke mwisho, (jina
tunalo) alisema baadhi ya wanafunzi wanaona ufahari kupelekwa shuleni
kwa pikipiki jambo linalowafanya wawe tayari kukubali kufanya ngono.
“Wapo wanafunzi wanaopenda kuonekana wanatoka
katika familia bora, ...hao ndiyo rahisi sana kuwapata, ukimpeleka
shuleni mara ya kwanza, mara ya pili basi umemaliza mchezo,” alisema
dereva huyo akijinasibu.
Alisema baadhi ya wanafunzi hutoka nyumbani kwao
wakiaga wanakwenda shuleni lakini badala yake hukutana na madereva wa
bodaboda ambao huwapeleka mafichoni na kufanya nao ngono.
Dereva mwingine wa bodaboda, mkazi wa Keko Machungwa, Elikunda
Kileo alikiri kuwepo kwa matukio hayo akisimulia kuwa mmoja wa madereva
wa bodaboda alipigwa na wananchi baada ya kukutwa akimtomasa mwanafunzi
wa shule ya sekondari akiwa ndani ya mabanda ya kutengenezea samani.
Kwa mujibu wa Kileo, dereva huyo alimhaidi
mwanafunzi kuwa angempeleka shuleni, lakini muda mfupi baadaye
alimwingiza kwenye banda la mafundi seremala na kuanza kumdhalilisha kwa
kumtomasa maeneo mbalimbali ya mwili wake.
“Jamaa aliingia na mwanafunzi kwenye banda la
mafundi seremala linalomilikiwa na kaka yake, cha kushangaza tuliona
anataka kufanya vitu vya ajabu, maana alianza kumshikashika yule binti,
ingawa binti mwenyewe hakuwa na wasiwasi wowote,” alisema Kileo na
kuongeza kuwa:
“Mafundi wakamwambia aondoke, lakini jamaa akaanza kuwatukana ndipo walipoamua kumpa kipigo.”
Dereva mwingine wa bodaboda anayefanya kazi Mbezi
Msumi alikiri kuwa na uhusiano na wanafunzi wawili na mwalimu mmoja
kutokana na kuwapa lifti ya pikipiki mara kwa mara.
“Si unajua tena kaka, mi ninao wawili, mmoja
kidato cha pili mwingine cha nne, tena nina mwalimu, wote nawachukua,
ingawa wakati mwingine naona aibu kuwa naye kwani yeye ni mkubwa kuliko
mimi,” alisema dereva huyo.
Hata hiyo, baadhi ya madereva wa bodaboda
waliwatupia lawama wanafunzi kuwa wao ndiyo wanaowashawishi madereva hao
kufanya nao ngono.
Renatus Kitwana dereva wa bodaboda anaefanya
biashara yake katika kituo cha Ukonga Mombasa, alisema baadhi ya
wanafunzi hufika kituoni hapo na kusimama muda mrefu wakiwasubiri ‘watu
wao’. “Kuna wanafunzi huja hapa kutafuta pikipiki, lakini wakiwakosa
watu wanaowataka watasubiri muda mrefu hadi jamaa watakaporudi kitu
kinachoonyesha kuwa nao wanapenda kufanya vitendo hivyo,” alisema
Kitwana.
Wanafunzi wananena
Agnes Tarimo, mwanafunzi aliyehitimu kidato cha
nne mwaka 2012 katika shule ya sekondari Jangwani, alisema kuwa kuna
baadhi ya wanafunzi wasichana walikuwa wanakwenda shuleni wakiwa na nguo
za kubadilisha kwenye mabegi yao kwa ajili ya kutoka shuleni na kuingia
mitaani bila kujulikana.
“Kuna wanafunzi wenzetu walikuwa wanabeba nguo za
kubadilisha kwenye mabegi yao. Jamaa wa bodaboda wakija wanakwenda nao
sehemu wanabadilisha nguo, halafu wanakwenda kufanya mambo yao huko
mafichoni,” alisema Agnes.
Naye Mwanaidi Seif mwanafunzi wa kidato cha Tatu,
shule ya sekondari Perfect Vision, alisema kuwa tamaa ya usafiri wa
bure (lifti) na chips imewafanya wanafunzi wengi kujihusisha na vitendo
vya ngono
“Wanafunzi wengi wanatamaa ya kupata vitu vizuri, wengi
wamejikuta wakifanya ngono na kupata mimba kwa kupenda kupewa lifti na
chipsi,” alisema Mwanaidi.
Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu
Anthony, Mbagala ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa
si msemaji wa shule, alisema kuwa suala la wanafunzi kuwa na uhusiano na
madereva siyo geni na kwamba lipo tangu siku nyingi.
“Ingawa hapa shuleni hatujapata kesi kama hiyo,
lakini suala hilo si geni lipo toka siku nyingi na siyo madereva wa
bodaboda tu wanaofanya vitendo hivyo hata madereva wa taxi na daladala,”
alisema mwalimu huyo. Alisema baadhi ya madereva wanaojihusisha na
‘mchezo’ huo ni watu wazima ambao umri wao ni sawa na wazazi wa
wanafunzi wanafanya nao ngono.
“Wengine ni watu wazima kabisa sawa na baba zao...
wazazi lazima wawaangalie sana watoto wao hali ni mbaya,” alisema
mwalimu huyo.
Wazazi walonga
Meshack Kilave, mkazi wa Tabata ambaye binti yake
anasomoma kidato cha kwanza kati shule ya sekondari Magomeni alisema
tatizo la wanafunzi kujihusisha kimapenzi na madereva lipo toka siku
nyingi na kwamba wanafunzi wanabuni mbinu mpya kila siku za kuwaficha
wazazi wao.
“Baadhi ya wanafunzi huaga nyumbani kuwa
wanakwenda kwenye masomo ya ziada kumbe wameshatekwa na jamaa wa
bodaboda,” alisema Kilave.
Alishauri wazazi kuwafuatilia kwa kuwauliza watoto wanapowabaini kumiliki vitu ambavyo hawakukinunua wazazi.
“Wazazi watawafuatilie watoto wao kwa karibu,
watabaini mambo mengi yaliyofichika, badala ya kukaa na kusikia
ukiambiwa mwanao ni mjamzito.”
Naye Stumai Ng’ingo, mkazi wa Kongowe alisema
ameshtushwa na taarifa za madereva wa bodaboda kufanya ngono na
wanafunzi akieleza kuwa ndio kwanza amezisikia taarifa hizo.
“Ndiyo ninasikia kwa mara ya kwanza kuwa madereva
wanaweza kufanya hivyo, sijui kama wadogo zangu wanaosoma sekondari
wanaweza kupona wasitumbukie mikononi mwa hao jamaa,” alisema Stumai.
George Daffa, mkazi wa Mtoni kwa Azizi Ali aliwatupia lawama baadhi ya
wazazi kuwa wanachangia watoto wao kufanya vitendo vibaya kutokana na
kukosa uangalizi wa kutosha.
“ Baadhi ya wazazi wanahitaji kubadilika, waache
tabia ya kudhani wakishawalipia watoto wao ada basi jukumu la
kuwafuatilia limeisha,” alisema Daffa
0 comments:
Post a Comment