ALIYEKUWA mchezaji wa Simba miaka kumi na tano iliyopita George Magere Masatu, amesema kuwa kwa sasa yuko tayari kurejea kwenye timu hiyo.
Masatu hivi sasa amerejea nchini akiwa tayari amestaafu soka lakini ana kadi ya uanachama wa timu hiyo yenye maskani yake Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Masatu amesema kuwa yuko tayari kurejea kama kocha na siyo mchezaji tena kama ilivyokuwa awali Masatu alisema kuwa, ana uwezo na uzoefu kufundisha aliyoupatia katika shule ya soka ya Arsenal huko Indonesia alikokuwa akicheza soka la kulipwa kwa zaidi ya miaka mitano.
“Kweli nimerudi nyumbani kuendelea na maisha, lakini ukisema kuhusu Simba mimi ni mwanachama.Na kama wakisema nifanye nao kazi,niko tayari haina shida
“Nimekuwa kocha kwenye shule ya watoto ya Arsenal kule Indonesia kwa zaidi ya miaka mitatu. Ninajua kazi inavyofanyika na wakisema wanataka tufanye kazi, basi tutafanya hivyo,” alisema Masatu aliyekuwa beki kisiki wakati wa enzi zake.
Masatu alianza kufanya vizuri akiwa na Pamba ya Mwanza kabla ya kujiunga na Simba mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Pamoja na kuwa na umbo dogo, Masatu alikuwa ndiye beki nyota na imara zaidi wa kati nchini na jina lake halijawahi kushuka chati pamoja na kuwa nje ya Tanzania kwa muda mrefu.
0 comments:
Post a Comment