Rais wa awamu ya tatu, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, alimpa Mrema nafasi ya Naibu Waziri Mkuu, kutokana na utendaji wake kuwa mzuri.
Kikwete alisema hayo alipokuwa akiwashukuru viongozi wa vyama vya siasa kwa kuwataja majina mmoja mmoja baada ya mwingine.
“Bila kumsahau Mrema ambaye hajalipwa mafao yake, Mrema ni Naibu Waziri Mkuu mstaafu ambaye hajalipwa mafao yake na bahati nzuri Mama Kombani uko hapa shughulikia mafao ya huyu mzee,” alisema Kikwete na kusababisha ukumbi mzima kulipuka kwa kicheko.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990 Mrema ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Vungo na Mwenyekiti wa chama cha TLP, alikuwa maarufu kutokana na umahiri wake wa utendaji kazi akiwa Mbunge wa Moshi Vijijini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mzee Mwinyi alimteua kushika nyadhifa mbalimbali kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na baadae Naibu Waziri Mkuu.
Baada ya kauli hiyo ya Rais, Mrema naye kwa utani alimjibu
“Mheshimiwa Rais nikilipwa mafao yangu hata hizi ndevu nitanyoa sasa,” alisema na kusababisha kwa mara nyingine ukumbi mzima kulipuka kwa kicheko.
Baadae alipohojiwa na waandishi,Waziri wa Utumishi wa Umma, Celina Kombani kuzungumzia utekelezaji wa agizo hilo la Rais unaanza lini aliwataka waandishi kuacha kufuatilia mambo binafsi ya watu.
Waziri Kombani hakuweka wazi stahiki ambazo Mrema anatakiwa alipwe kwa kile alichodai kuwa mafao ya mtu ni siri na hawezi kuzungumzia hilo kwa kuwa maadili hayaruhusu.
“Nyie waandishi ninawashangaa sana mmekosa kitu cha kuandika? Mbona hamuhoji mafao ya watu wengine kama ya Mzee Mwinyi mafao ya mtu ni siri siwezi kusema juu ya hilo kwa nitakuwa nimekiuka maadili,”alisisitiza Kombani.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk.Benson Bana alisema Rais kumwagiza Waziri mwenye mamlaka husika kushughulikia mafao hayo siyo kwamba ni tiketi ya kulipwa.
Alisema Waziri katika utekelezaji wake ataangalia Sheria inasema nini na kisha atamwandikia Rais kwa kumshauri kwamba agizo lako haliwezi kutekelezwa kwa sababu mbalimbali kwa kuwa cheo hicho hakiko katika katiba .
Dk. Bana aliongeza kuwa Waziri atamwandikia Rais kumjulisha kuwa mhusika hana mafao anayodai kwa kuwa alishalipwa akiwa Waziri pamoja na yale ya ubunge.
0 comments:
Post a Comment