Matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka 2012, yameendelea
kuitikisa sekta ya elimu nchini baada ya shule kufunguliwa jana bila
kutangazwa kwa waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu.
Kwa kawaida, wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na
kidato cha tano na vyuo vya ualimu, hutangazwa mapema ili kutoa fursa
kwa wanafunzi na shule husika kufanya maandalizi ya mahitaji.
Lakini tofauti na ilivyozoeleka, wanafunzi wa
kidato cha sita walianza masomo yao jana huku wale wanaotarajiwa
kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ualimu wakiwa hawajatangazwa.
Mkanganyiko huo pia unazigusa shule za sekondari
za binafsi kwani baadhi zilishachukua wanafunzi wa kidato cha tano na
nyingine ziliahirishwa kufunguliwa jana kutokana na kutokuwa na
wanafunzi hao.
Hali hiyo imewaacha njia panda baadhi ya wakuu wa
shule ambao waliwaambia waandishi wetu kwa nyakati tofauti kwamba
wanasubiri maelekezo ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu
suala hilo, huku wengine wakitishia kufunga shule hizo na kuzigeuza kuwa
vyuo vya taaluma nyingine.
Akitangaza matokeo mapya ya kidato cha nne Mei
mwaka huu, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
aliahidi kwamba majina ya watakaojiunga na kidato cha tano yangetangazwa
mapema ili wapate muda wa kujiandaa na kuripoti kwenye shule husika
mapema kadri itakavyowezekana.
Jana, Dk Kawambwa hakupatikana kuzungumzia suala
hilo na msemaji wa Wizara hiyo, Bunyanzu Ntambi alisema suala la
kutangaza majina hayo lipo kwenye ngazi za uamuzi.
“Sababu hasa siwezi kujua, lakini kwa kuwa matokeo
yenyewe yalichelewa kutangazwa ni rahisi hata mchakato wa kutangaza
waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano uchelewe,” alisema Bunyanzu.
Wakuu wa shule
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Morogoro, Thomas Chihwalo alisema: “Ninachosubiri ni maelekezo ya wizara, nini kifanyike.”
Mkuu wa Sekondari ya Azania, Dar es Salaam, Benard
Ngoyaye alipoulizwa alisema: “Nenda kwa Ofisa Elimu wa Wilaya, yeye
anafahamu kwa nini majina yamechelewa kufika wakati
walikwishachaguliwa.”
Mkuu wa Shule ya Sekondari Arusha, Christopher
Malamusha alisema walitarajia wizara ingetangaza majina hayo mapema
lakini hadi jana walikuwa hawajapokea taarifa zozote.
Mkuu wa Sekondari ya Tambaza aliyejitambulisha kwa
jina moja, Zuberi naye alisema wanasubiri maelekezo ya Ofisa Elimu
Wilaya ya Ilala.
Hata hivyo, Ofisa Elimu ya Sekondari wa Manispaa ya Ilala,
Germana Mng’aho alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo na kwamba
mhusika mkuu ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Mkuu wa Shule ya
Sekondari ya Ilboru, Arusha, Julius Shula alisema hata majina ya
wanafunzi wanaojiunga na shule yao hawayafahamu.
Mmoja wa walimu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani,
Dar es Salaam, alisema kwa kawaida wanafunzi wa kidato cha tano
huripoti shuleni wiki mbili kabla ya wale wa kidato cha sita kitu
ambacho mwaka huu kimekuwa tofauti.
Msaidizi wa Mkuu wa Shule ya
Sekondari Bwiru Wavulana ya Mwanza, Malongo Charles alisema wanasubiri
wanafunzi watakaopelekwa na Serikali.
Hata hivyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Moshi, Fanuel Angalo alisema anaamini wizara husika itatangaza wiki hii.
“Ni jambo jipya kidogo limetokea lakini tunaamini
Waziri atatoa tangazo lake wiki hii halafu wanafunzi hao wa kidato cha
tano waripoti shuleni wiki ijayo,” alisema Angalo.
Mkoani Tanga, walimu katika Shule za Sekondari za
Tanga Ufundi, Gallanos na Usagara kwa nyakati tofauti, waliilalamikia
wizara kwa kuwachelewa kuwapelekea wanafunzi wa kidato cha tano na
kusema kuwa hiyo imevuruga utaratibu wa ufundishaji.
Hakuna athari
Baadhi ya wadau wa elimu walisema kilichotokea si
kigeni kwani kimepata kutokea miaka ya nyuma na mihula ilirekebishwa na
kwenda sawa na wenzao ambao walikuwa wameanza masomo.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Ushauri wa
HakiElimu, Nyanda Shuli alisema kubadilika kwa muhula wa kuanza masomo
si jambo kubwa ambalo linaweza kuathiri elimu na kwamba anaamini wizara
itakuwa imetoa mwongozo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema si mara ya kwanza kwa muhula wa masomo
kubadilika kwani imewahi kutokea siku za nyuma na marekebisho yakafanywa
ili kufidia muda ambao wanafunzi wanakuwa wamepishana na wenzao.
“Sidhani kama ni jambo kubwa sana ambalo linaweza
kuathiri chochote katika masuala ya elimu, la msingi ni kuhakikisha kuwa
waliochelewa kuanza masomo wanapata muda wa kumaliza mtaala (mtalaa) wa
masomo kama inavyotakiwa.”
Kwa siku tatu mfululizo, kuanzia Juni 29, mwaka
huu, wakuu wa shule za sekondari za Serikali walikutana katika Chuo cha
Ufundi, Arusha kupitia majina ya waliochaguliwa na kuiachia kamati ya
kukamilisha kazi hiyo.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya kikao hicho
zinasema tatizo kubwa lilikuwa ni idadi ya wanafunzi kuwa ndogo
ikilinganishwa na nafasi za kidato cha tano kutokana na kufeli kwa
wanafunzi wengi katika matokeo ya kidato cha nne, 2012.
Hata baada ya matokeo hayo kufanyiwa marekebisho, idadi ya wenye sifa za kuchaguliwa ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi.
Mara nyingi, wanafunzi walio katika nafasi kubwa
ya kuchaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano ni wale waliofaulu
kwa daraja la kwanza mpaka la tatu.
Kwa sasa shule za Serikali zenye
kidato cha tano zina uwezo wa kuchukua wanafunzi 45,000 kwa wakati
mmoja.
Baada ya matokeo ya kidato cha nne kurekebishwa,
wanafunzi waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu ni 35,349;
daraja la kwanza ni 3,242, daraja la pili ni 10,355 na daraja la tatu
ni 21,752.
Ikiwa wanafunzi hao wote watachaguliwa kujiunga na kidato cha
tano, bado shule hizo zitakuwa na upungufu wa zaidi ya wanafunzi 9,000.
Upungufu huo hautakuwa na athari kwa shule hizo
pekee, bali hata kwa vyuo vya ualimu na vile vya kati ambavyo hupokea
wanafunzi waliohitimu kidato cha nne na kufaulu.
Mwaka jana, wanafunzi
31,516 walichaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule 201 za
Serikali.
Idadi hiyo ni karibu asilimia 60 ya shule 495
ambazo kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Mitihani la Taifa (Necta),
zilifanya mitihani ya kidato cha sita mwaka huu. Takwimu hizo pia
zinaonyesha kuwa idadi ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa kufanya
mtihani huo ni 43,231.
Kwa maana hiyo, ikiwa shule za Serikali
zitachagua idadi sawa na ile ya mwaka jana, (31,516) kwa ajili ya
kujiunga na kidato cha tano, shule binafsi 294 zitalazimika kugawana
wanafunzi 3,833 watakaobaki.
Shaka ya wadau
Kutokana na idadi ya wanafunzi wanaofaulu mtihani
wa kidato cha nne kuendelea kushuka kila mwaka, Mwenyekiti wa Chama cha
Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo
alisema asilimia 70 ya shule zenye kidato cha tano zimefungwa ama
kupunguza idadi ya wanafunzi.
Mringo alisema matokeo ya hali hiyo yanaonekana
kwenye yale ya kidato cha sita yaliyotangazwa Mei 31, mwaka huu ambayo
baadhi shule kongwe zilizokuwa zinafanya vizuri miaka ya nyuma,
zilishika nafasi za mwisho akisema hali hiyo imekuwapo kwa miaka minne
mfululizo.
“Shule za private (binafsi) asilimia 70 ama
wamefunga au wamepunguza udahili wa wanafunzi, kwa ufupi wameanza
kujitoa kwenye hii bishara ya shule, shule kama ya Green Acres na St.
Mary’s kushika nafasi za mwisho ni kiashirio cha kuwa walishaanza
kujitoa kwenye hiyo biashara,” alisema.
Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Raida, Profesa
Ruth Meena alisema wameamua kutochukua tena wanafunzi wa kidato cha
tano kuanzia sasa na baada ya walio kidato cha sita kuhitimu,
wanafikiria kuifanya taasisi hiyo kuwa chuo.
Meneja wa shule hiyo, Anneth Meena alisema: “Kila
mwaka idadi ya ufaulu inashuka na wanafunzi wa kujiunga na kidato cha
tano wanakosekana, sisi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu walikuwa
ni ishirini na kitu na wanaoingia kidato cha sita sasa hivi ni 21.”
Alisema wakati hali ikiwa hivyo miundombinu ya
shule hiyo yenye kidato cha tano na sita pekee ina uwezo wa kuchukua
wanafunzi zaidi ya 400.
Hofu vyuo vikuu
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar es
Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema kwa jinsi hali ilivyo siku
zijazo kutakuwa na upungufu mkubwa wa wanafunzi wenye sifa za kwenda
vyuo vikuu.
Alisema kutokana na matokeo ya kidato cha nne
mwaka 2012, alitegemea kuona bajeti ya elimu kwa mwaka 2013/14
inajielekeza kutatua matatizo yanayojulikana na yale yatakayoainishwa na
Tume ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kitu ambacho hakijafanyika.
“Nilitegemea resources (rasilimali) nyingi
zingeelekezwa kwenye kutatua matatizo ya elimu yanayojulikana na yale
yasiyojulikana, lakini bajeti ya elimu ni ndogo kama miaka mingine,
wakati ya Kenya ikiwa ni asilimia 18 na Uganda ikikaribiana na hiyo
kwetu ni asilimia 10,” alisema na kuongeza:
Msemaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU),
Edward Mkaku alisema kufeli kwa wanafunzi wengi ngazi za shule siyo
sababu ya kufanya vyuo hivyo vifungwe kwani taasisi hizo zina kazi kuu
tatu ambazo ni kufundisha, kufanya utafiti na kushauri.
Alisema pia kuwa, TCU imeanzisha programu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuruhusu hata watu walioishia darasa la
saba na kufanya kazi muda mrefu kwenye maeneo mbalimbali kujiunga na
vyuo vikuu.
“Kuna mtu alimaliza darasa la saba na akaenda
kusoma cheti cha sheria, huyu mtu kafanya kazi kama karani wa Mahakama
ya hakimu mkazi kwa miaka minane, huyu mtu ukimwingiza kusoma sheria na
mwanafunzi aliyetoka kidato cha sita lazima afanye vizuri zaidi,”
alisema.
CHANZO:GAZETI LA MWANANCHI