Pages

 

Monday, July 8, 2013

MOS DEF ATOA VIDEO MAALUM YA MWEZI WA RAMADHAN JUU YA WAFUNGWA GUANTANAMO BAY

0 comments

Wakati mwezi mtukufu wa Ramadhan unazidi kusogea,zaidi ya wafungwa 100 wanaoshikiliwa katika gereza la Guantanamo Bay wamekuwa wanaendelea na mgomo wao wa kula.Katika  taarifa za siri iliyovuja kutoka gerezani hapo,zaidi ya wafungwa 40 wamekuwa wakilishwa kwa kutumia mabavu,kwa maagizo ya jeshi la nchi hiyo

Katika video hii ya dakika 4 iliyoandaliwa na taasisi ya haki za binadamu,muongozaji wa filam Asif Kapadia na Yasin Bey ambae anajulikana zaidi kama Mos Def muigizaji na mwanamuziki  kutoka Marekani inaonesha jinsi wafungwa hao wanavyolazimishwa kula kwa kutumia nguvu.

Viongozi wa Jumuia ya Kiislam wameitaka serikali ya Rais Barack Obama kufikiria upya juu ya uamuzi huo wa kuwalisha wafungwa kwa kutumia mabavu,hasa wakati huu wa mfungo wa Ramadhan.

Serikali ya Marekani ilisema kuwa ili kuzuia dharura inayoweza kutokea hapo baadae au matatizo katika wajibu wao, itaheshimu funga ya mchana  kwa kuwalisha kwa nguvu wafungwa 45 wakati wa usiku.Lakini vikundi mbalimbali vya kiislam vimesema kuwa kuendelea kutumia mtindo huo wa kulazimisha kula wakati wa mwezi wa Ramadhan ni sawa na kutia chumvi kwenye kidonda.

"Katika imani yetu ni kosa kumlazimisha mtu kula wakati wowote ule,lakini inaumiza kuona mambo haya yanafanywa hata mwezi wa Ramadhan"Amenukuliwa akisema Ibrahim Hooper msemaji mkuu wa kikundi kinachosimamia haki za Waislam nchini Marekani.The Council On American-Islamic Relations(CAIR).

"(Ni kosa) sio tu kwa mujibu wa imani za kiislam bali pia kitendo hiki kinakiuka misingi ya haki za binadamu kimataifa na hata kanuni za kitabibu"

Dakta Azzam Tamimi kiongozi wa jamii ya Waislam nchini Uingereza amesema "Tunatarajia serikali ya Marekani italifikiria upya suala hili.Mwezi wa Ramadhan unavyoanza suala hili litazidi kuleta fedheha kwa watawala wa Marekani.Ni wakati muafaka Rais Obama afanye maamuzi ya kijasiri kulishughulikia katika njia ambayo itaeleweka na jumuia za kiislam duniani kote.

Wafungwa wanne kati ya 106 waliogoma kupinga kitendo cha serikali ya Marekani kuwaweka kizuizini muda mrefu bila ya kuwafungulia mashtaka, wamefungua kesi katika mahakama za huko Marekani, kupinga kulishwa kwa nguvu.

Kesi iliyofunguliwa katika mahakama ya Washington wiki iliyopita inapinga kulishwa kwa nguvu usiku kwani mgomaji anaweza asinywe maji na kuhatarisha maisha ya alielishwa kwa nguvu.

Katika kuadhimisha mwanzo wa mwezi mtukufu,kikundi cha Haki za Binadamu kimetuma video maalum kwa gazeti la The Guardian la Uingereza.

Ndani ya video hiyo Repa na Muigizaji maarufu wa Marekani Mos Def ambae alisilimu na sasa anaitwa Yasin Bey anaonekana kama mfungwa akiingia kwenye chumba maalum cha Guantanamo Bay kwa ajili ya kwenda kulishwa na madaktari ambao wanatumia mirija ya kulishia wagonjwa mahututi.

MosDef katika video hii anaonesha taabu wanayoipata wafungwa wanaopitia zoezi hili la kulishwa kwa nguvu.

Nyota huyo wa filam za kimarekani,anasema alijitolea kukubali kuingizwa mirija hiyo, kama inavyoonekana, kwa kushirikiana na madaktari wawili ambao nao walijitolea kukamilisha igizo hilo.

Video hiyo inayodumu kwa dakika nne inajaribu kutoa taswira halisi ya kinachotokea ndani ya gereza hilo lililopo kisiwani, katika bahari ya Atlantiki jirani na nchi ya Cuba,kufuatia taarifa za siri ya kufanyika kwa zoezi hilo kuvuja kwa televisheni ya al-Jazeera.

Katika nyaraka za kijeshi zilizovuja kutoka gerezani hapo na kutumwa kwa al-Jazeera ambayo ina kichwa cha habari`Medical management Standard Operating Procedure `inafafanua kuwa ili mfungwa aitwe mgomaji,anatakiwa awe hajala angalau milo tisa na awe amepungua uzito kwa asilimia 85 ya uzito wake wa kawaida.

Iwapo mfungwa analazimika kulishwa kwa nguvu,madaktari wanajeshi walio ndani ya gereza hilo watamfunga minyororo na mdomoni atawekewa kifaa maalum katakachomdhibiti mfungwa huyo asing`ate au kutema mate.Na baada ya hapo,mirija ya chakula huzamishwa tumboni kwa kupitia matundu ya pua.

Zoezi hili huchukua takriban dakika 20 hadi 30,lakini mfungwa analazimika kubaki kwenye kiti huku kafungwa,kwa masaa hadi mawili hadi atakapopigwa X-Ray kifuani ili kufahamu iwapo chakula kimetua tumboni mwa mfungwa.

Baada ya hapo mfungwa huku akiwa na minyororo anapelekwa kwenye chumba kidogo `kikavu`ambako ataendelea kuchungwa na mlinzi kwa saa nzima ili asitapike au kujaribu kujitapisha.Endapo atatapika,anarudishwa tena kwenye kiti kuanza tena zoezi la kumlisha.

Na endapo mfungwa atang`ata mrija wa chakula,madaktari watakibana kicwa chake bila kuachia hadi pale mfungwa atakapo legeza mdomo wake

Makundi ya waumini wa dini zingine pia wamelaani zoezi hilo.Mwezi uliopita mchungaji Richard Pates mwenyekiti wa Kamati ya Sheria za Kimataifa na Amani katika Muungano wa Wachungaji wa Kikatoliki nchini Marekani,alimuandikia barua Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel kumkumbushia malalamiko ya  Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu dhidi ya kitendo cha kuwalisha wafungwa kwa kutumia mabavu

Sehemu ya barua hiyo inasema;"Badala ya kutumia mbinu hizo,kwanza taifa letu lifanye kila liwezalo kushughulikia adha inayopelekea mgomo huo kufanyika" 

0 comments:

Post a Comment

 
Said Nuhu © 2012 SAID NUHU BLOGS. BLOG IMETENGENEZWA NA BongoClan blog designer nipigie 0658184797