Pages

 

Friday, July 26, 2013

VYAMA VYA USHIRIKA NI MAGENGE YA WEZI-KIKWETE

0 comments
Rais Kikwete
Bukoba. Rais Jakaya Kikwete, amesema baadhi ya vyama vya ushirika nchini vina mkusanyiko wa wezi wanaokula fedha za wananchi bila hata kunawa.
Kikwete aliyasema hayo juzi jioni alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kufungua jengo la kitega uchumi la Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Kagera (KCU), mjini Bukoba.
“Acheni kuwa wachuuzi tu wa kununua na kuuza mazao ya wananchi na badala yake mjiingize katika shughuli za uwekezaji na maendeleo ya kwelikweli ya wanachama wenu,” alinena Rais.
“Hapa Kagera ni kitovu cha ushirika na KCU ni kitovu cha kuboresha na kuleta usasa katika shughuli za ushirika. Siyo kama vyama vingine ambavyo ni mkusanyiko wa wezi wanaokula waziwazi mchana bila hata aibu ….wanakula bila kunawa,” alisisitiza.
Rais Kikwete alisema huko nyuma Serikali ilifanya uamuzi wa kulipa madeni yote ya ushirika nchini ili kuvipunguzia vyama mzigo wa kujiendesha.
Alisema hata hivyo sasa vyama hivyohivyo, vimeanza kujitumbukiza tena katika madeni na kwamba hiyo inatokana na kukosa viongozi waaminifu na waadilifu.
Kabla ya kuzindua jengo hilo, Rais Kikwete aliweka jiwe la msingi kwenye upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba ambao unapanuliwa ili kuufanya kuwa wa kisasa. Kazi hiyo itagharimu Sh21.015 bilioni, itakapokamilika.
Mradi huo wa upanuzi wa uwanja ulianza Februari mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Februari mwakani.
Upanuzi huo ukikamilika uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuhudumia wasafiri 500,000 kwa mwaka sawa na wasafiri 150 kwa saa.
Uwanja huo umekuwa ukilalamiwa kuwa ndiyo kikwazo cha kukosekana kwa huduma za uhakika za usafiri wa anga kati ya Kagera na mikoa mingine nchini.
Kwa sasa wananchi wengi wa mkoa huo wanaosafiri lwa ndege, wamekuwa wakiishia katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza na baadaye kusafiri kwa meli.

0 comments:

Post a Comment

 
Said Nuhu © 2012 SAID NUHU BLOGS. BLOG IMETENGENEZWA NA BongoClan blog designer nipigie 0658184797