Pages

 

Sunday, July 7, 2013

MABOMU YA MACHOZI YAITIKISA DAR

0 comments
JESHI la Polisi jijini Dar es Salaam, jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi maeneo ya Manzese, kuwatawanya wafanyabiashara wadogowadogo (Machinga) waliogoma kupisha ujenzi unaoendelea wa mabasi yaendayo kasi (DART).
Polisi  wakiwa katika magari yao waliwatawanya wafanyabiashara hao waliokuwa wamegoma kutoka kutokana na kudai kuwa eneo hilo ni muhimu kwao kwa ajili ya kuendeshea biashara.
Wakiwa na silaha mbalimbali, ikiwemo za moto, walifanikiwa kuwatawanya wafanyabiashara hao kwa kutumia mabomu ya machozi.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa operasheni hiyo ilianza tangu wiki iliyopita, kutokana na ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama, pamoja na familia yake.

 Operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara hao ilianza jana asubuhi na ilikwenda vizuri, baadaye baadhi ya askari walipungua na kubaki wachache, hapo ndipo wafanyabiashara walipopata mwanya wa kurudi barabarani na kufunga barabara kwa kuweka mawe ili magari yasipite.

“Kosa lilikuwa ni kupunguza askari, hapo ndipo wafanyabiashara tulijikusanya na kuweka mawe ili askari wasipite kuja kutuzuia wala magari yasipite,” alisema askari aliyeshudia.

Mtu mwingine aliyejitambulisha kwa jina Juma Mohamed, alisema wanashangaa askari kuendelea na operasheni hiyo kwa kuwa kama ni ujio wa Obama ulishapita, hivyo waruhusiwe kurudi katika maeneo hayo.

Magari ya Makamanda wa Polisi (OCD) wa vituo mbalimbali, ikiwemo Kimara na Kinondoni, yakiwa na Makamanda wao, yalikuja kuongeza nguvu, huku gari jingine la polisi likiwasomba waliokamatwa katika oparesheni hiyo.

Aidha, maeneo ya kuanzia Darajani mpaka soko la Manzese kulikuwa kumewekwa mawe barabarani, huku barabara inayojengwa ikiwa imevunjwa katika baadhi ya maeneo kutokana na vurugu hizo.

Maeneo hayo yote palikuwa kimya, tofauti na siku zote ambapo kunakuwa na biashara mbalimbali zikiendelea, huku polisi wakiwaaamuru watu wanaopita kutembea kwa mwendo wa haraka pamoja na kutosogelea eneo la tukio.

Pia maduka yote katika maeneo hayo yalikuwa yamefungwa na baada ya muda wa mapambano hali ilianza kutulia kuanzia saa 9:00 alasiri.

Operasheni hiyo inaelezwa kulenga kuwaondoa wafanyabiashara wadogowadogo ili kuweza kupisha ukamilishaji wa ujenzi wa Barabara ya Morogoro, inayojengwa kwa ajili ya mabasi yaendayo kasi (DART).

0 comments:

Post a Comment

 
Said Nuhu © 2012 SAID NUHU BLOGS. BLOG IMETENGENEZWA NA BongoClan blog designer nipigie 0658184797