Pages

 

Monday, July 8, 2013

WATANO WAANGAMIA MGODINI MERERANI

0 comments
Watu watano wamefariki dunia katika vilima vya mgodi wa Mererarni, na mtu wa sita alikimbizwa hospitali ya KCMC Moshi akiwa mahututi,baada ya kuangukiwa na kifusi cha shimo walilokuwa wakifanya kazi.
Tukio hilo lilitokea alfajiri ya jana Jumapili,katika Wilaya ya Simanjiro ,Mkoa wa Manyara,ambapo inadaiwa kuwa watu hao sita walikuwa wakifanya kazi katika shimo la mgodi wa Tanzanite,linalomilikiwa na Bwana Onesmo Mbise  mkazi wa mjini Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoani Manyara Bw.Akili Mpwapwa,alithibitisha kutokea kwa tukio hilo,na kusema kuwa ni kawaida wafanyakazi katika mgodi huo kuendesha shughuli zao nyakati za usiku,na kuongeza kuwa polisi  wanaendelea kulifuatilia tukio hilo.
Kamanda Mpwapwa,alithibitisha vifo vya watu hao ambao aliwataja kwa majina kuwa ni Jackson Kavishe,Noel Kilwa-Kitui,Emmanuel John,Godlove Zebhlon na Emmanuel Joshua,ambao walikwenye eneo la tukio baada ya kuangukiwa na kifusi cha shimo walilokuwa wakifanya kazi.
Mfanyakazi wa sita ametajwa kuwa ni Siphael Simba,ambae alikutwa hai na waokoaji waliofika kwenye shimo hilo lililosajiliwa kwa jina la kampuni ya madini ya Fanon.
Simba alikimbizwa katika Hospitali ya KCMC mjini Moshi ambako alikuwa akiendelea kupigania maisha yake.
Wachimbaji kwenye mgodi huo wamekiri kuwa wanapenda kufanya shughuli zao usiku kwa kuwa hali ya hewa huwa tulivu isiyo na joto kali,tofauti na mchana,ambayo joto huwa kali hasa katika eneo linalokabiliwa na ukame wa mvua.
Matukio ya kuporomoka kwa mashimo ya mgodi ni ya kawaida huko Mererani,ambapo matukio mawili ya kutisha yalitokea mwaka 1998 na 2008 na watu 100 kuangamia katika kila tukio.
Hata hivyo matukio hayo yalisababishwa na maporomoko ya maji yaliyotoka na mvua kubwa za masika katika miezi ya Machi na Aprili
 .

0 comments:

Post a Comment

 
Said Nuhu © 2012 SAID NUHU BLOGS. BLOG IMETENGENEZWA NA BongoClan blog designer nipigie 0658184797