Pages

 

Wednesday, July 17, 2013

VITAMBULISHO VYA TAIFA:MAMLAKA YAANZA KUCHUKUA ALAMA ZA VIDOLE,SAINI NA PICHA

0 comments
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imeanza zoezi la kuchukua alama za vidole vyote kumi, kupiga picha na kuweka saini ya kielektroniki kwa wakazi wa Wilaya ya Temeke tayari kwa kutoa vitambulisho hivyo.
Kaimu Mkuu wa Mawasiliano na Machapisho, Thomas William aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, kutokana na wingi wa watu katika Jiji la Dar es Salaam, zoezi hilo limegawanywa katika ngazi ya wilaya hadi wilaya.
“Hili zoezi tumelianza juzi, tunachukua alama za vidole kumi, kupiga picha na kuweka saini za kielektroniki kwa wakazi wa Temeke, tumeanzia Kigamboni na kutokana na ukubwa wake tumeigawanya kwa kanda saba,” alisema.
  William alisema,  kanda ya kwanza inahusisha mitaa yote katika kata za Kimbiji, Pemba Mnazi, Kigamboni, Vijibweni, Kibada, Mji Mwema, Somangila, Kisarawe 11, Tungi na mitaa ya Mtoni Kijichi, Mgeni nani na Misheni iliyoko katika Kata ya Kijichi.
Alisema, ili kuboresha mwonekano mzuri wa picha kwenye kitambulisho hicho, mwombaji anashauriwa kutokuvaa nguo nyeupe, kijivu, bluu mpauko, pinki na kofia au kapelo wakati wa kupiga picha.
Aidha, William aliwataka waajiri wa mashirika mbalimbali kuwaruhusu watumishi kushiriki katika zoezi hilo siku watakayokuwa wamepangiwa ili kurahisisha zoezi hilo na kuepuka usumbufu wa kurudia eneo.
“Tunawaomba waajiri katika mashirika mbalimbali nchini wawaruhusu watumishi wao kufika katika eneo muhimu kwa kuzingatia tarehe aliyopangiwa ili kufanikisha zoezi. Hata wale ambao walikuwa hawajajaza fomu za kujiandikisha wanatakiwa kufika katika kata zao ikiwa zoezi linafanyika katika halmashauri hiyo,” alisema William.
Alisema, zoezi hilo limetoa kipaumbele kwa makundi maalumu ya walemavu na wazee wasiojiweza na kuwa walemavu wa mikono watapigwa picha bila kuchukuliwa alama za vidole.
Katika Jiji
la Dar es Salaam, zoezi hilo limeanzia Wilaya ya Temeke, likifuatiwa na Ilala na kumalizikia Kinondoni

0 comments:

Post a Comment

 
Said Nuhu © 2012 SAID NUHU BLOGS. BLOG IMETENGENEZWA NA BongoClan blog designer nipigie 0658184797