Elizabeth Michael wakati akifikishwa mahakama ya Kisutu wakati kesi yake ikiwa katika hatua za awali |
Mahakama Kuu
Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imekubali kusikiliza ombi la kufanya uchunguzi
wa umri wa msanii wa filamu nchini, Eizabeth Michael (18) ‘Lulu’, anayekabiliwa
na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, marehemu Steven Kanumba (28).
Mahakama hiyo imesema itasikiliza maombi hayo Juni 25, mwaka
huu, baada ya pande zote mbili kuwasilisha vielelezo kuhusiana nayo.
Uamuzi huo ulitolewa asubuhi ya Jumatatu na Jaji Dk. Fauz Twaib baada ya
kutokea mabishano ya kisheria kati ya upande wa utetezi na Jamhuri kuhusu Mahakama
kuchunguza umri halisi wa mshitakiwa kati ya miaka 18 iliyoandikwa kwenye hati
ya mashitaka na miaka 17 kama inavyodaiwa na upande wa utetezi.
Jaji alisema kuwa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini
Dar es Salaam, ilikosea kukataa kuchunguza umri wa mshitakiwa na kuamua
kufutilia mbali amri iliyotolewa na Hakimu Augustina Mmbando.
Hakimu Mmbando alikataa kuchunguza umri wa Lulu na Mahakama
Kuu imechukua jalada lake na itafanya yenyewe uchunguzi huo.
Alisema mawakili wa utetezi Florence Massawe na Peter
Kibatala watawasilisha kwa njia ya maandishi vielelezo Jumatano na upande wa
Jamhuri utajibu kwa njia hiyo ya maandishi Juni 20, mwaka huu na Mahakama
kusikiliza Juni 25, 2012.
Katika kesi ya msingi, Lulu anadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka
huu katika eneo la Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, alimuua Kanumba.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya
Jinai (CPA), Lulu, hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Hata hivyo, baada ya upelelezi kukamilika, itahamishiwa
katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Mapema Jumatatu saa 3:45 asubuhi, Lulu, alifikishwa katika
viunga vya mahakama hiyo akiwa chini ya ulinzi wa askari magereza.
Msanii huyo alikuwa amevaa suruari ya jeans rangi nyeusi na
blauzi nyeusi pamoja na kikoti maarufu kama `kibajaji` cha rangi ya zambarau huku
akionekana kujiamini tofauti na awali alipokuwa akifikishwa mahakamani.
0 comments:
Post a Comment