Pages

 

Tuesday, June 12, 2012

KESI YA LULU:MAHAKAMA KUU YAFUTA AMRI YA MAHAKAMA YA KISUTU KUHUSU CHETI CHA KUZALIWA

0 comments

Elizabeth Michael wakati akifikishwa mahakama ya Kisutu wakati kesi yake ikiwa katika hatua za awali

Mahakama  Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imekubali kusikiliza ombi la kufanya uchunguzi wa umri wa msanii wa filamu nchini, Eizabeth Michael (18) ‘Lulu’, anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, marehemu Steven Kanumba (28).

Mahakama hiyo imesema itasikiliza maombi hayo Juni 25, mwaka huu, baada ya pande zote mbili kuwasilisha vielelezo kuhusiana nayo.

Uamuzi huo ulitolewa asubuhi ya Jumatatu na Jaji Dk. Fauz Twaib baada ya kutokea mabishano ya kisheria kati ya upande wa utetezi na Jamhuri kuhusu Mahakama kuchunguza umri halisi wa mshitakiwa kati ya miaka 18 iliyoandikwa kwenye hati ya mashitaka na miaka 17 kama inavyodaiwa na upande wa utetezi.


Jaji alisema kuwa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, ilikosea kukataa kuchunguza umri wa mshitakiwa na kuamua kufutilia mbali amri iliyotolewa na Hakimu Augustina Mmbando.

Hakimu Mmbando alikataa kuchunguza umri wa Lulu na Mahakama Kuu imechukua jalada lake na itafanya yenyewe uchunguzi huo.

Alisema mawakili wa utetezi Florence Massawe na Peter Kibatala watawasilisha kwa njia ya maandishi vielelezo Jumatano na upande wa Jamhuri utajibu kwa njia hiyo ya maandishi Juni 20, mwaka huu na Mahakama kusikiliza Juni 25, 2012.

Katika kesi ya msingi, Lulu anadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu katika eneo la Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, alimuua Kanumba.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), Lulu, hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Hata hivyo, baada ya upelelezi kukamilika, itahamishiwa katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Mapema Jumatatu saa 3:45 asubuhi, Lulu, alifikishwa katika viunga vya mahakama hiyo akiwa chini ya ulinzi wa askari magereza.

Msanii huyo alikuwa amevaa suruari ya jeans rangi nyeusi na blauzi nyeusi pamoja na kikoti maarufu kama `kibajaji` cha rangi ya zambarau huku akionekana kujiamini tofauti na awali alipokuwa akifikishwa mahakamani.

0 comments:

Post a Comment

 
Said Nuhu © 2012 SAID NUHU BLOGS. BLOG IMETENGENEZWA NA BongoClan blog designer nipigie 0658184797