Pages

 

Wednesday, June 13, 2012

MAENDELEO YA HALI ZA WASANII `SAJUKI` NA `VENGU`

0 comments
MSANII maarufu wa filamu  Tanzania ambae alikuwa ameenda  India kwa ajili ya matibabu, Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ameanza  kupata nafuu na  anaendelea na dozi ili aweze kupona kabisa.
Akiongea na waandishi wa magazeti ya kampuni  ya Global Publishers siku  ya Jumatatu  nyumbani kwake Tabata jijini Dar Es Salaam, msanii huyo alisema sasa hivi afya yake imeimarika kidogo tofauti na ilivyokuwa awali na anawashukuru watu wote waliojitolea kwa namna yoyote ile kwa lengo la kumsaidia na kwamba yeye hana cha kuwalipa ila Mungu atawalipa

.
“Nina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwani hali yangu inaendelea vizuri, kinachonisumbua ni ukali wa hizi dawa tu kwani kuna wakati mwingine nakosa nguvu lakini madaktari waliniambia nizitumie mpaka zitakapoisha,” alisema Sajuki na kuongeza:
“Pia niwashukuru Watanzania kwa michango yao, hakika wameonesha ubinadamu wa hali ya juu kwangu lakini pia ningependa nikanushe taarifa za kwamba nimerejea kama nilivyokwenda. Kwa aliyeniona wakati naondoka atakubaliana na mimi kuwa afya yangu imetengemaa kwa kiasi fulani.”
Mbali na shukrani kwa Watanzania, Sajuki amewashukuru pia madaktari wa hospitali ya Saifee,mjini Mumbai,India kwa uangalizi waliompatia ikiwemo kumpa chakula kizuri kilichokuwa kikihitajika kutokana na dawa anazotumia
.
“Nawashukuru sana wale madaktari kwani wamenitibu chini ya uangalizi mzuri kiasi cha kunifanya nipate nafuu hii,” alisema
.
Sajuki alianza kusumbuliwa na uvimbe mwaka jana ulioanzia mkononi kisha ndani ya mwili kwenye ini na baadae ikagundulika kuwa, siyo kwenye ini tu bali umesambaa hadi sehemu nyingine za tumboni.
..
 WAKATI afya ya  Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ ikiendelea vizuri baada ya kupata matibabu habari kutoka huko huko nchini India zinasema kuna utata juu ya maendeleo ya afya ya mchekeshaji maarufu nchini, Joseph Shamba ‘Vengu’ ambaye naye yuko nchini humo kwa matibabu, 


 Habari  zinadai kuwa hali ya msanii huyo wa kundi la wachekeshaji la Orijino Komedi imekuwa ya giza mbele ambapo ndugu zake waishio Dar hawajui nini kinaendelea.
 
Katikati ya mwezi Mei, ilidaiwa Vengu angerejea nchini wakati wowote baada ya afya yake kutengemaa, lakini ndugu mmoja wa karibu  amesema ilishindikana kuruhusiwa baada ya hali ya msanii huyo kubadilika ghafla.


“Ilikuwa arudi nyumbani kweli, maana kidogo alikuwa anaridhisha, lakini ghafla hali ikabadilika tena, kwa hiyo hatarudi kwa sasa,” alisema ndugu huyo
.
  Vengu aliwahi kulazwa kwa muda mrefu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) akikabiliwa na ugonjwa uitwayo  Cerebral Atrophy. Ugonjwa huu husababisha seli za kichwani kukosa mawasiliano na sehemu nyingine na mgonjwa hupoteza fahamu mara kwa mara.
Akiwa hospitali ya Muhimbili, hali ilizidi kuwa mbaya hivyo mchekeshaji huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Apolo iliyopo nchini India kwa matibabu zaidi.
  
Sajuki alikwenda Mumbai, India katikati ya Mei mwaka huu kutibiwa matatizo ya uvimbe tumboni kwenye Hospitali ya Saifee. Alirejea nchini Juni 6, mwaka huu, akiwa anaendelea vizuri.

0 comments:

Post a Comment

 
Said Nuhu © 2012 SAID NUHU BLOGS. BLOG IMETENGENEZWA NA BongoClan blog designer nipigie 0658184797