Pages

 

Friday, June 22, 2012

KWAMBA LULU NI MKUBWA MAWAKILI WA SERIKALI WAWASILISHA VIELELEZO MAHAKAMA KUU

0 comments
Lulu alipofikishwa mahakama kuu Juni 11 mwaka huu
MAWAKILI wa Serikali jana waliwasilisha vielelezo Mahakama kuu kupinga maelezo ya upande wa utetezi kuwa umri wa msanii wa kike wa filamu  Tanzania Elizabeth Michael ni mdogo

Habari zinasema kuwa vielelezo hivyo vya Jamhuri ni Mkanda wa video aina ya CD, yenye mahohjiano kati ya mshtakiwa huyo na mtangazaji mmoja nchini. Vingine ni maelezo ya mshtakiwa huyo aliyoyatoa polisi wakati alipohojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, maombi ya hati ya kusafiria (Passport) na maombi ya leseni ya udereva.

 Awali vielelezo hivyo walitakiwa kuviwasilishwa juzi, lakini ilishindikana na badala yake vikawasilishwa jana na kesi itaendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo, Juni 25.

Msanii Elizabeth Michael ambae hujulikana zaidi kwa jina la Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kumuua msanii mwenzake, Marehemu Steven Kanumba aliyefariki dunia nyumbani kwake Sinza, April 7, 2012.

Hata hivyo katika hatua za awali za kesi hiyo, umri wake ulizua utata baada ya mawakili wanaomtetea Lulu kudai kuwa bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyoonesha.

Hivyo mawakili hao walilazimika kuwasilisha maombi mahakamani kuiomba mahakama iruhusu ufanyike uchunguzi wa umri sahihi wa mshtakiwa huyo na ikiridhika kuwa ni mtoto basi kesi yake iendeshwe kwa misingi ya kesi za watoto kisheria ili kulinda maslahi yake.

 Juni 11, 2012 Mahakama Kuu ilikubali  kufanya uchunguzi huo yenyewe kwa lengo la kubaini usahihi wa umri wa mshtakiwa huyo na ikaziagiza na kuzipangia tarehe pande zote katika kesi hiyo kuwasilisha mahakamani hapo vielelezo watakavyovitumia katika hoja zao.

 Jopo la mawakili wanaomtetea Lulu likiongozwa na Kennedy Fungamtama Juni 13 waliwasilisha mahakamani hati za viapo vya wazazi wake na vielelezo vingine kikiwemo cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo vinavyoonesha kuwa bado ni mtoto.

 Lakini taarifa zilizopatikana mahakamani hapo zinaeleza kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na Jamhuri vinaonesha kuwa mshtakiwa huyo ni mtu mzima kwa kuwa kwa mujibu wa vielezo hivyo ana umri zaidi ya miaka 18.

Viapo vya wazazi wa mshtakiwa huyo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Peter Kibatala ambaye ni mmoja wa mawakili wanaomtetea Lulu vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa miaka 17.

Viapo hivyo ni kiapo cha mama yake Lulu Lucresia Augustin Kalugila, mkazi wa  Dar eS Salaam na kiapo cha baba mzazi Michael Kimemeta, mkazi wa Moshi.

Viapo  vyote vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa April 16, 1995  katika kituo cha Afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba B.0318479 cha Julai 23, 2004.
 
Pia viapo hivyo vinaeleza kuwa baada ya kuzaliwa mshtakiwa,  mama yake alimpa jina la Diana Michael Kimemeta, lakini alimpeleka mtoto huyo Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ndugu zake, walimpa jina la Elizabeth, jina la bibi yake Elizabeth Shikana.

Viapo hivyo vinaendelea kueleza kuwa baada ya majadiliano wote, yeye mama, baba na ndugu wengine walikubaliana kuwa wamuite Diana Elizabeth Michael Kimemeta .

“ Elizabeth Michael Kimemeta alibatizwa katika Kanisa la Katoliki  Chang’ombe Septemba 28, 1997 na alichukua majina ya ubatizo Diana Elizabeth Michael Kimemeta;” inasomeka sehemu nyingine ya kiapo hicho cha mama wa mshtakiwa.

Utata wa umri wa mshtakiwa huyo uliibuka Mei 7, 2012 katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya wakili wake Fungamtama kudai kuwa ana miaka 17 na hivyo kuomba kesi yake isikilizwe katika mahakama ya watoto.

Hata hivyo Mahakama ya Kisutu iliyakataa maombi hayo ikisema kuwa haina mamlaka ya kuyashughulikia na kushauri maombi hayo yawasilishwe Mahamaka Kuu.

Ndipo Mei 15 wakili Kibatala aliwasilisha maombi hayo mahakama kuu wakiomba mahakama hiyo iamuru kwamba Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kisheria kushughulikia maombi hayo.
Katika maombi hayo namba 46 ya mwaka 2012,  pia mawakili hao waliomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kufanya wala kuagiza uchunguzi huo ufanyike, basi Mahakama Kuu yenyewe ama iagize au ifanye uchunguzi huo.

Sambamba na hayo pia waliomba Mahakama Kuu iamuru mwenendo wa kesi ya msingi katika Mahakama ya Kisutu usimamishwe hadi suala la umri litakapopatiwa ufumbuzi.

Katika uamuzi wake Jaji Dk. Fauz Twaib alisema kuwa Mahakama ya Kisutu ina mamlaka ya kushughulikia maombi hayo na kwamba ilikosea kukataa kuyashughulikia.

Pia Jaji Dk. Twaib  alikubaliana na hoja za pingamizi la awali la wajibu Maombi(Jamhuri) kupitia kwa Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro akisaidiana na Wakili Elizabeth Kaganda, walizozitoa wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, Mei 28,2012.

 Wakili Kimaro alidai kuwa maombi hayo yamewasilishwa mahakamani hapo kinyume cha sheria na kwamba hata vifungu vilivyotumika katika madai hayo haviipi Mahakama Kuu uwezo wa kuyashughulikia.
 
 Hata hivyo licha ya kukubali kuwa maombi hayo yaliwasilishwa mahamakani isivyo sahihi, lakini Jaji Dk. Twaib alisema bado Mahakama hiyo ina mamlaka ya kuyashughulikia.

 Chini ya kifungu cha 44 cha Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi, Jaji Dk. Twaib aliuagiza upande wa mwombaji(mawakili wanaomtetea mshtakiwa), kuwasilisha mahakamani hati hizo za viapo na vielelezo vya umri wa mshtakiwa huyo juzi Jumatano.



0 comments:

Post a Comment

 
Said Nuhu © 2012 SAID NUHU BLOGS. BLOG IMETENGENEZWA NA BongoClan blog designer nipigie 0658184797