WIKI mbili baada ya kifo cha aliyekuwa msanii nyota wa filamu nchini,
Steven Kanumba, wazazi wake; Charles Musekwa Kanumba na Mama yake,
Flora Mutegoa ambao hawaishi pamoja, wametofautiana kuhusu suala la mali
na mirathi.
Juzi, Mzee Kanumba aliibuka na kudai kuwa kuna kundi
la watu linalomdanganya mama huyo wa marehemu kwamba linajua zilipo mali
za Steven jambo ambalo alisema ni uongo na kumtaka awe na subira na
asidanganyike.
Hata hivyo,kauli hiyo imepingwa na Mutegoa ambaye
amehoji sababu za mumewe huyo kuzungumzia mali za mwanaye wakati huu.
Alidai kuwa Mzee Kanumba hajawahi kuwa na mawasiliano na marehemu tangu
mwaka 1999 alipoondoka kwao, Shinyanga.
Akizungumza katika
mahojiano maalumu juzi, Mzee Kanumba alimsihi mkewe
kutodanganyika kwa kuwa yeye akiwa baba mzazi wa Kanumba anajua mali
zote za mtoto wake na ndiye pekee anayeweza kumtendea haki katika
kuzigawa.
“Mali za marehemu mwanangu nazifahamu zote, kwa hiyo
hakuna shaka tutazigawa kwa sababu hakuna baba mwingine na haki yangu
ipo palepale hakuna atakayeinyang’anya,” alisema na kuongeza:
“Nisingependa
tuwape watu faida ya kuanza kuvutana mahakamani, tunatakiwa suala hili
tulimalize sisi wenyewe kama tulivyompata mtoto wetu. Ninasisitiza mali
zote zisifanyiwe vurugu ziachwe kama zilivyo.”
Katika kuthibitisha
kwamba anazijua mali hizo, mzee huyo alisema Steven ameacha magari
matatu, Sh40 milioni, viwanja viwili na akaunti mbili za benki na
Kampuni ya Filamu.
Akerwa na tambiko
Mzee Kanumba alisema
anasikitishwa na tambiko la Kihaya lililofanyika katika kaburi la mtoto
wake, jambo ambalo alisema halikutakiwa kwa kuwa marehemu alikuwa
Mkristo na alizikwa kwa imani hiyo.
“Mimi ni Mkristo, mtu
aliyezikwa Kikristo huwezi tena kuanza kumfanyia mambo ya kipagani na
kuanza kumtambikia, hiyo kwetu hairuhusiwi,” alisema Mzee Kanumba na
kuongeza:
“Hata hivyo, marehemu alikuwa Msukuma, si Mhaya, itakuwaje
wamtambikie Kihaya na kumwaga pombe aina ya rubisi huku marehemu alikuwa
hatumii pombe na mimi pia situmii pombe?”
Kuhusu tambiko, Flora
alisema hakuna kitu kama hicho kilichofanyika kwenye kaburi la mwanaye
isipokuwa Wahaya wana mila zao kwa mwenzao aliyepatwa na msiba.
“Kilichofanyika
siyo tambiko bali, ni mila zetu za Kihaya. Unapofiwa wenzako
wanakuletea vitu kama kreti ya soda, bia na mkungu wa ndizi. Lile siyo
tambiko ni mila tu, mimi pia ni Mkristo, siwezi kushiriki matambiko,”
alisema.
Alisema suala hilo la kugawa mali au msimamizi wa
mirathi walitakiwa kukutana pande mbili, yaani yeye na mkewe baada ya
kupita siku 20 tangu alipozikwa waangalie namna ya kugawa huku
akisisitiza kuwa hakuna mtu mwingine anayeruhusiwa kuingilia masuala
hayo.
Mama amkana
Kwa upande wake, Mutegoa ambaye sasa bado
yupo nyumbani kwa Kanumba, Sinza Vatican, Dar es Salaam alisisitiza
kwamba marehemu hajawahi kuwasiliana na baba yake huyo tangu mwaka 1999.
Alieleza
kushangazwa na taarifa hizo kutoka kwa mzazi mwenzake huyo na
kusisitiza kuwa ni mapema mno kuanza kujadili mali za mtoto.
“Nasikitika
kulisema hili kwani bado niko kwenye msiba wa mwanangu. Hata hivyo,
sidhani kama mwenzangu anajua chochote kuhusu Steven, achilia mbali mali
zake, hawajawahi kuwa na ukaribu mpaka kuweza kujua mali zake,” alisema
na kuongeza:
“Hata hivyo, mbona anazungumzia mali tu, hivi
anafahamu kama Steven alikuwa na madeni? Ninamsihi aachane na hizo
habari kwa wakati huu kwani hazina uzito wowote ukilinganisha na thamani
ya mtoto niliyempoteza,” alisema.
CHANZO CHA HABARI-THE CHOICE