Pages

 

Wednesday, May 9, 2012

HAKUNA KUWAHURUMIA,MAWAZIRI LAZIMA WASHTAKIWE;CCM YATAMKA

0 comments



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakitakuwa na huruma kwa mawaziri ambao wamewajibishwa kutokana na wizara zao kutajwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwamba zimehusika na ufisadi, badala yake kitakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanafikishwa mahakamani

Kauli hiyo imekuja kipindi ambacho tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inafanya uchunguzi dhidi ya mawaziri sita ambao wametajwa kwenye ripoti hiyo ya CAG na ambao Rais Jakaya Kikwete aliwang’oa katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.
William Mganga Ngeleja

Lucy Sawere Nkya
“Kama uchunguzi wa Takukuru utathibitisha tuhuma hizo, watapanda kizimbani kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria,” Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana.

Akitolea mfano wa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kupanda kizimbani juzi kutoa ushahidi kwenye kesi inayomhusu aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, Nape alisema: “Hii inathibitisha kuwa hakuna aliye juu ya sheria za nchi.”

Nape alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa chama hicho, mjini Dodoma ambako pamoja na mambo mengine, alitangaza ratiba ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec).

“Katika hilo nasema kuwa hakuna aliye juu ya sheria, jana (juzi) Mzee Mkapa alipanda mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi, iweje hao wengine waachwe? Nasema kama walihusika na ikathibitika kweli hata kama wengine wamebaki katika baraza, ni lazima watawajibika,’’ alisema.

Mawaziri walioachwa katika baraza hilo jipya ni Mustafa Mkulo (Fedha), Mhandisi Omary Nundu (Uchukuzi), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii) na William Ngeleja (Nishati na Madini).

Lazaro Samuel Nyalandu
Wengine waliokuwa wakitajwa kuguswa katika ripoti ya CAG ni George Mkuchika aliyekuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi na Profesa Jumanne Maghembe aliyuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika. Mawaziri hao sasa wamehamishwa katika wizara hizo. Mkuchika sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora) na Profesa Maghembe ni Waziri wa Maji.

Nape alikiri kupata taarifa za mawaziri hao wa zamani kuchunguzwa na Takukuru, lakini akasema katika mtego huo si wote ambao wanaweza kunaswa.
Dr. Cyril August Chami
Kuhusu wabunge wa CCM waliotia saini barua kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ikiwa ni shinikizo la kutaka mawaziri hao wajiuzulu au wawajibishwe, Nape alisema chama chake hakifikirii na hakitathubutu kuwajadili.

Akizungumzia ratiba ya kikao hicho, alisema Kamati ya Maadili ya CCm itakutana Jumamosi ijayo chini ya Uenyekiti wa Rais Kikwete na baadaye siku hiyohiyo, Kamati Kuu itakutana.

Mustafa Haidi Makunganya Mkulo
Alisema Mei 13, itakuwa ni siku ya semina kwa wajumbe wa Nec ambayo pamoja na mambo mengine, watapata nafasi ya kuipitia Katiba mpya ya CCM pamoja na marekebisho.

Jumatatu ya Mei 14, kutakuwa na kikao cha Nec ambacho  kitajadili mustakabali wa siasa nchini pamoja na mabadiliko ya Katiba ya nchi.

Mawaziri waanza kazi
Mawaziri wapya jana walianza kazi baada ya kukabidhiwa na watangulizi wao ambao ama waliondolewa kwenye nafasi zao, au walihamishiwa wizara nyingine.

Mawaziri wapya waliokabidhiwa ofisi jana ni William Mgimwa (Fedha), Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Dk Fenella Mukangara (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo) na Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika).

Omari Rashid Nundu
Katika makabidhiano hayo, Dk Mukangara aliwataka watendaji wa wizara hiyo kuhakikisha kuwa wanasimamia uwajibikaji na nidhamu ili kutimiza mpango wa miaka mitano.

Akizungumza na wafanyakazi wa wizara hiyo, Dk Mukangara alisema kila mfanyakazi ana wajibu wa kuhakikisha kuwa anatimiza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kujua anachokifanya akiwa kazini.

“Suala la uwajibikaji ni muhimu kwa sababu kila mmoja anajua wajibu wake, hivyo basi hapaswi kusukumwa,” alisema Dk Mukangara.

Waziri wa Fedha, Willim Mgimwa pamoja na manaibu wake, Janeth Mbene na Saada Mkuya Salumu waliahidi kusimama imara kuhakikisha kodi za Serikali zinakusanywa kikamilifu.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda hakutaka kuzungumza lolote kwani alisema alikuwa na majukumu mengi ya kufanya katika ofisi yake hiyo mpya.

Wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria waliwapokea mawaziri wao kwa mbwembwe. Waziri wake, Mathias Chikawe alirejea tena wizarani hapo akitokea Ofisi ya Rais (Utawala Bora) na jana aliingia akiwa na naibu wake, Angela Kairuki.

Wizara ya Maliasili na Utalii, imeandaa sherehe ya kumuaga aliyekuwa Waziri wake, Ezekiel Maige na kumkaribisha Balozi Khamis Kagasheki.

Msemaji wa wizara hiyo, George Matiko alisema  wataandaa sherehe hiyo kuonyesha upendo waliokuwa nao kwa waziri aliyepita.

Matiko alisema wasingependa kumuaga Maige kimyakimya hivyo kwa kuandaa sherehe ambayo itaonyesha ni jinsi gani walikuwa karibu naye.

Jana, Maige alifika wizarani hapo na kukabidhi ofisi kwa Balozi Kagasheki.
SOURCE :Mwananchi Communicatios

0 comments:

Post a Comment

 
Said Nuhu © 2012 SAID NUHU BLOGS. BLOG IMETENGENEZWA NA BongoClan blog designer nipigie 0658184797